Na Penina Malundo, timesmajira
SERIKALI ya Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha rasilimali za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria zinalindwa ili zinufaishe jamii zinazozunguka ziwa hilo na mataifa husika kwa ujumla.
Pia inaendelea kudhibiti matumizi ya zana haramu za uvuvi, kupiga marufuku uvuvi wa samaki wachanga, kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi na kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya Ziwa Victoria bila kuathiri mazingira.
Hii ni kutokana na vitendo vya uvuvi haramu ambavyo vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki ndani ya ziwa hilo kutokana na mazalia ya samaki kuharibiwa na sumu ama vifaa ambavyo havitakiwi katika uvuvi.
Kutokana na hali hiyo serikali na wadau mbalimbali wanafanya jitihada za kuhakikisha vitendo hivyo haramu vinatokomezwa na kumalizwa kabisa kwa kutumia njia mbadala za kulinda mazingira katika ziwa hilo ili kunusuru maisha ya watu karibu milioni 120 wanaotumia Ziwa Victoria kutoka Tanzania, Uganda, na Kenya.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Utafiti wa Mazingira la ACCORD-Tanzania,ulibainisha kuwa kuna hatari ya kutoweka kwa aina zote za samaki katika Ziwa Victoria miaka zaidi ya 30 ijayo, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na uvuvi haramu.
Katika utafiti wa shirika hilo la ACCORD, unaonesha kuwa ifikapo mwaka 2048 kutakuwa na upungufu mkubwa wa samaki katika ziwa hilo kwani uzalishaji wake nchini umeshuka kwa asilimia 50, kutoka tani 400,000 hadi tani 200,000, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Mbali na mikakati mbalimbali inayowekwa na serikali katika kupambana na uvuvi haramu katika mialo inayozunguka Ziwa Victoria,bado Kitengo cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Mwambao Mwa Ziwa na Bahari (BMU),vimekuwa ni vitengo vizuri vya kupambana na uvuvi haramu.
Licha ya jitihada hizo zinazofanywa na BMU lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupambana na vitendo vya uvuvi haramu ikiwemo utumiaji wa silaha za jadi katika doria zao kwa lengo la kujilinda wanapokuwa wanalinda mialo yao.
Changamoto hiyo imekuwa inawarudisha nyuma kiufanisi na kufanya watumishi wa kitengo hicho kupunguza kasi ya ufanyaji kazi kutokana na kukosa rasilimari ya vitendea kazi ambavyo vinakuwa msaada kwao katika ufanyaji wa doria.
Katibu wa BMU Mwalo wa Butuja wilayani Ilemela Mkoani Mwanza,Maneno Khamis anasema shughuli zinazofanywa na kitengo chao cha BMU ni kuwasimamia wavuvi kama watumiaji muhimu wa ziwa katika shughuli zao za uvuvi na kuhakikisha wanavua samaki kwa njia halali.
Anasema BMU haina silaha za kuhakikisha wavuvi haramu wanawadhibiti katika mialo yao, ila mara nyingi wanachukuliwa na maofisa uvuvi wa wilaya au kata katika kufanya misako yao ya kawaida hivyo kufanya vitendo vya uvuvi haramu kuendelea kushika kasi.
Khamis anasema ukamataji wa wavuvi haramu mara nyingi unakuwa usiku wa saa saba au saa nane kwani ndio muda ambao wavuvi wengi wanakuwa wapo kazini kwaajili ya kuvua samaki na mida hiyo inapaswa wao kuwa makini kwa kujiami na kuwa na silaha ambazo zinaweza kuwasaidia kupambana nao.
”Tunaona ni namna gani sato na sangara wanavyotoweka sasa,hii inasababishwa na uvuvi haramu unaofanywa na baadhi ya wavuvi ambao wanatumia makokoro,baruti,betri za solar na sumu hali inayowakimbiza samaki na kuharibu mazalia yao,”anasema na kuongeza
”Sasa wavuvi hao hatuwezi kuwapata mchana hata kidogo,wanaingia usiku kazini hivyo tunahitaji kuwa makini nao katika kuwakamata,sisi BMU ambao ndo tunatengemewa katika hii mialo unakuta tuna silaha za jadi kama panga na nondo tunaenda kuzuia uhalifu huku ukiangalia kazi hii ni ya kujitolea katika kuhakikisha tunalinda samaki wasitoweka,”.
Anasema wakisema BMU iombe doria kwa jeshi la polisi hawawezi kukubali kwa sababu watakwambia hawana bajeti ya mafuta hivyo operasheni hiyo inakufa na kutozaa matunda huku wavuvi hao wakiendelea kutumia njia haramu katika kuvua samaki.
”Kazi hii hatulipwi ni kujitolea,inatuwia vigumu kwa changamoto hizi tunazokumbana nazo kwani zimekuwa zinatuumiza katika kupambana na hawa waharifu,”anasisitiza.
***Akizungumzia hatua ambazo Serikali zinaweza kusaidia vikundi vya BMU
Khamis anasema kutokana na serikali kuendelea kupambana na uvuvi haramu,vikundi vyao vingeweza kusaidiwa na kupewa nguvu ya kusimamia katika kupambana na uvuvi huo kwenye Ziwa Victoria.
Anasema inashangaza kuona Serikali ipo lakini haitoi nguvu ya rasilimari katika vikundi hivyo na kufanya kushindwa kuendelea na ulinzi ambao wamekuwa ukifanywa kama yalivyokuwa malengo ya kuanzishwa kwa BMU.
Ambapo anasema serikali haijatoa nguvu kwa vikundi vyao inawaacha tu,wanaingia katika doria wakiwa hawana vitu vya kujihami na wavuvi haramu, ukizingatia kazi hiyo ni ya kujitolea.
“Tunaomba Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuangalia vikundi vyetu na kuviwezesha hata kuvipa mafunzo ya namna ya kupambana na huu uvuvi haramu ambao umekuwa ukiwatoesha samaki na kukimbia na mazalia kuuliwa,”anasema.
Kwa Upande wake mmoja wa wavuvi wa mwalo wa Kanyenze wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Juma Said(Sio jina lake halisi) anasema wanatumia kokoro kuvulia samaki kutokana na kifaa hicho kutokuwa na gharama kubwa katika matengenezo yake kuliko kutumia mashine.
Anasema kwa sababu wao ni wavuvi wadogo na hawana mitaji ya kununulia mashine kubwa inawalazimu kutumia kokoro kuvua samaki pia wamekuwa wanarithi vifaa hivyo kutoka kwa watangulizi wao ambao miaka ya nyuma walikuwa wanatumia.
”Wavuvi wanaotumia kokoro katika Ziwa Victoria wengi wao wanakuwa wamerithi kutoka kwa watangulizi wao pia kutumia mashine katika kuvua samaki inagaharama kubwa sana kununua inafika hadi milioni 20,”anasema
Amekiri kuwa ni kweli utumiaji wa kokoro ni mbaya kwani uvuaji wake uanzia chini na kusababisha mazalia ya samaki kuvurugika.
Sanjari na hayo anaiomba serikali kuwasaidia wavuvi hao kwa kuwakopesha fedha kupitia vikundi ili kuweza kununua mashine za kuvulia samaki na kuacha kutumia kokoro kwani kwa sasa samaki wa ziwa victoria wamekuwa wamekimbia tofauti na miaka ya zamani.
”Serikali itakapotusaidia sisi wavuvi wadogo ili tumiliki mashine za kuvulia tutashukuru sana, tutaacha kukimbizana na hawa watu wa BMU ambao wamekuwa wakitukamata mara kwa mara kutokana na kutumia kokoro kuvulia samaki ambayo imepigwa marufuku,”anasema.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika