November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tutuba:Mkafanye kazi kwa kufuata sheria

Josephine Majura WFM, Arusha

 Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba amelitaka Baraza la Uongozi la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wakati wa utekelezaji wa majukumu yake, kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Sera, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa.

 Bw. Emmanuel Tutuba alitoa wito huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), uliofanyika katika ukumbi wa Chuo hicho jijini Arusha.

 “Tuna imani na ninyi na nimatumaini yetu kwamba mtatumia weledi wenu kwa uadilifu katika kutekeleza majukumu mliyopewa ili kuhakikisha kwamba, Chuo chetu kinakua na kinakidhi matarajio tuliyojiwekea” alisema Bw. Tutuba”.

Alilitaka Baraza hilo kuhakikisha wanashirikiana na  Menejimenti ya Chuo kusimamia matumizi ya fedha za Serikali ikiwa ni pamoja na mali za Chuo zinazo hamishika na zisizohamishika, ili kufikia malengo makubwa waliojiwekea.

Sambasamba na uzinduzi wa Baraza hilo Bw. Tutuba alitembelea maeneo ya Chuo hicho ambapo alijonea miundombinu mbalimbali chuoni hapo na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazokikabili Chuo hicho ikiwemo uhaba wa makazi kwa wanafunzi.

Bw. Tutuba aliahidi kufanyia kazi changamoto ya makazi kwa wanafunzi ambao asilimia 90 wanakaa nje ya maeneo ya Chuo ili kuhakikisha wanafunzi hao wanaishi chuoni ili wawe karibu na mazingira ya chuoni.

“Nimetembea na nimeona ujenzi unaoendelea hivyo, naahidi kulifanyia kazi ombi lenu la kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa makazi ya wanafunzi wetu  alisema Bw. Tutuba”.

Alitoa wito kwa Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote wa Baraza la Uongozi kwa kuteuliwa kwao kuwa wasimamizi wa shughuli za Chuo, aliwataka wakawe chachu ya kuchochea uzalendo na utumishi wa umma kwa Chuo hicho.

“Nitumie nafasi hii pia kuwakaribisha kwenye familia ya Wizara ya Fedha na Mipango.  na  matarajio yangu mtatekeleza majukumu yenu kwa ushirikiano wa karibu na Wizara pamoja na Taasisi nyingine ili kuhakikisha mipango tuliyojiwekea inafikiwa”, alisema Bw. Tutuba”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Dkt. Mwamini Tulli, aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kushirikiana katika kutimiza majukumu waliyopewa kwa mujibu wa sheria katika kipindi chote cha miaka mitatu watakayokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Cairo Mwaitete amesema kuwa Chuo kimeendelea kuhakikisha kina miundombinu wezeshi ili vijana wasome katika mazingira bora na salama chuoni pamoja na kuhakikisha IAA inaendelea kutoa elimu bora.