May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfuko wa SELF MF wampongeza Rais Samia

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MFUKO wa Kifedha wa Self (Self Microfinance Fund), umempongeza Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Hassan Suluhu kwa kutimiza mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani akichukua nafasi ya Hayati John Pombe Magufuli.

Akizungumza na Wanahabari Dar es Salaam leo (Machi 11, 2022), Mkurugenzi Mtendaji wa Self MF, Mudith Cheyo, alisema kuwa kuna mambo mengi na makubwa kwa nchi yetu yaliyofanywa na Mama Samia, akiendeleza na kuboresha zaidi yale yaliyoanza kufanywa na mtangulizi wake, kuanzia katika nyanja za ustawi wa jamii, siasa, miundombinu, uchumi na mengineyo mengi, akitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Manejimenti na Wafanyakazi wa Mfuko wa SELF, tunajivunia kuwa sehemu ya Watanzania waliomsaidia Mama Samia kutekeleza Ilani ya CCM katika suala zima la kuwainua Watanzania kiuchumi. Kwa kutambua ugumu uliokuwapo awali wa kupata mikopo, tumekuwa tukitoa mikopo kwa masharti nafuu, tukiwafikia wale ambao hawakuwa wakifikiwa na taasisi mbalimbali za kifedha.

“Sambamba na hilo, tumekuwa tukitoa huduma zetu hata kwa wananchi wa kawaida wasio na leseni za biashara huku tukiwapa elimu ya jinsi ya kujiendeleza zaidi na kukuza biashara zao,” alisema Cheyo.

Alisisitiza kuwa katika kuhakikisha wanawafikia Tanzania wengi zaidi, wamefungua matawi katika maeno mbalimbali ya Tanzania katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Dodoma, Mwanza, Arusha, Zanzibar, Kahama na Mbeya.

“Tawi la Dar es Salaam ambalo lipo katika jengo la Sukari, likihudumia Dar es Salaam, Pwani, Mtwara na Lindi; huku lile la Arusha lililopo jengo la Hazina Ndogo, likihudumia Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Tawi la Dodoma lililopo jengo la Chuo cha Biblia, linahudumia Dodoma, Morogoro na Singida; tawi la Mbeya lililopo jengo la NSSF linahudumia Mbeya, Songwe, Iringa, Ruvuma, Rukwa, na Njombe na tawi la Mwanza lililopo jengo la Posta, linahudumia Mwanza, Simiyu na Mara.

“Tawi la Zanzibar lililopo jengo la Posta Kijangwani, linahudumia Zanzibar na Pemba; tawi la Kahama linahudumia Shinyanga, Katavi na Tabora; Tawi la Geita lililopo mtaa wa Bombambili, linahudumia Kigoma, Geita na Kagera,” alisema.

Alisema katika matawi yao hayo, wamekuwa wakitoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, zikiwamo taasisi mbalimbali za kifedha, haya yote yakiwezekana kutokana na uongozi thabiti wa Mama Samia ambaye Serikali yake imewatengenezea mazingira mazuri na rafiki yaliyoturahishia kuwafikia kirahisi wadau wao (wafanyabishara) kupitia utaratibu uliowekwa wa kuwatengea maeneo maalum ya kuendesha biashara zao, ikiwamo majukwaa mbalimbali yanayoandaliwa ili kuwapa elimu.

“Wanafamilia wa Mfuko wa SELF, tunaona fahari mambo kadhaa tuliyoyafanya ndani ya kipindi hiki cha uongozi wa Rais Samia tukiwa tumeanzisha bidhaa/huduma zinazowawezesha Watanzania kupata mkopo wenye masharti nafuu, tukiwalenga Mama Lishe, Machinga na wafanyabiashara wadogo wadogo ili kuwaondolea umaskini.

“Mikopo yetu imekuwa ya riba nafuu ili kila mmoja aweze kuimudu, lengo likiwa ni kumsaidia Rais wetu Mama Samia kuwaondolea Watanzania umaskini,” alisisitiza Cheyo.
Alisema kuwa katika kuhakikisha wanawafikia Watanzania wengi zaidi, wanatarajia kuongeza matawi mengine kumi (10) katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, lakini pia wakipanga kutoa huduma zetu kwa njia ya kidijitali ili kuwafikia wengi zaidi wenye uhitaji wa mikopo ili kuinua biashara zao.

Alisema kwamba kutokana na mafanikio waliyoyapata, wameweza kurejesha kwa jamii kwa kutoa msaada wa vitanda 80 na magodoro yake katika Chuo cha Walemavu cha Yombo, Dar es Salaam, vyote vikiwa na thamani ya Tshs 29,390,600.00.

Huu ni Mfuko ulioanzishwa Septempa 2014 kwa lengo kuu la kutekeleza sera za Serikali katika uwezeshaji Wananchi kiuchumi kwa kutoa suluhisho la upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi wenye kipato cha chini hususan waishio vijijini.

Mfuko wa SELF, hadi kufikia Desemba, 2021 umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya TZS 257.9 bilioni kwa wakopaji 187,731 pamoja na kuendelea kutoa mikopo kwa taasisi mbalimbali (Wholesale loans).

Mfuko huo umefanikiwa kuanzisha huduma mbalimbali ambazo zinamlenga moja kwa moja muhusika (Retail products) kama vile mikopo kwa ajili ya wajasiliamali wadogo na wa kati (MSMEs), mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo (Group loans) na mikopo kwa wafanyakazi wa Serikali. Huduma hizi zitaleta mapinduzi makubwa sana katika kumuinua Mtanzania wa kawaida kimapato hatimaye kukuza ustawi wa jamii na kuimarisha uchumi wa Taifa.