Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu ameweka bayana kuwa pamoja na mambo mengine, ACT Wazalendo kinataka Katiba Mpya ili kuweka misingi imara ya kulinda haki za kisiasa na kiraia.
Ndugu Ado ameyasema hayo akitoa salamu za Vyama vya Siasa kwenye Maadhimisho ya Miaka 10 ya Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF, Dar es salaam leo tarehe 13 Mei 2022.
“Ni kweli uwanja wa kisiasa (political space) na kiraia (civic space) umeanza kufunguka. Leo hii, THRDC wasingeweza kufanya shughuli kama hii miaka michache iliyopita kwa sababu Akaunti zao za Benki zilifungiwa. Kwa hili, tunampongeza Mh. Rais”
“Hata hivyo, ACT Wazalendo hatutaki suala hili liendelee kuwa hisani ya Mh. Rais. Tunataka Katiba Mpya ili iweke misingi madhubuti ya kisheria kulinda haki za kisiasa, kiuchumi na kiraia”- alisisitiza Ndugu Ado Shaibu.
“ACT Wazalendo tunataka Mchakato wa Katiba Mpya uanze sasa sambamba na mchakato wa Tume Huru ya Uchaguzi. Watetezi wa Haki za Binadamu tunapaswa kuungana kwenye hili”- Aliongezea Ndugu Ado Shaibu.
Awali Ndugu Ado aliwapongeza THRDC kwa kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na kwa kazi kubwa wanayoifanya.
“THRDC mnafanya kazi kubwa sana ya kuwatetea watetezi wa haki za binadamu. Sisi wanasiasa ni sehemu ya wanufaika kwa kupaza sauti kwenu au msaada wa kisheria. Kwenye Ripoti yenu ya Miaka 10, kuna matukio Kama ya Kutekwa kwa Raphael Ongangi (Aliyekuwa Msaidizi wa Ndugu Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama), kutekwa kwa Ndugu Abdul Nondo (Mwenyekiti wa Vijana), kukamatwa kwa Ndugu Vital Maembe (Naibu Msemaji wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa, Ubunifu na Michezo).
Kwenye matukio yote haya mmefanya kazi kubwa ya kupaza sauti na kutoa msaada wa kisheria. Endeleeni na mapambano kwa kasi zaidi”- Alisisitiza Ndugu Ado Shaibu.
More Stories
Balozi Kombo :Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu nishati yakamilika, Marais 25 kuhudhuria
Mbunge Mavunde awawezesha kiuchumi wafanyabiashara soko la Sabasaba Dodoma
Msama: Geor Davie ni mtumishi wa kweli