May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya madini yaja na mikakati mipya ukusanyaji wa maduhuli

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

KAMISHNA wa Tume ya Madini, Prof. Abdulkarim Mruma, amesema kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, mwaka hhuu ni kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023-2024, Tume imeidhinisha maombi mapya ya leseni za madini 7596.

Hiyo ni asilimia 100 ya maombi yaliyowasilishwa kama mkakati wa kuendelea kutoa fursa zaidi za uwekezaji katika Sekta ya Madini ili wananchi wanufaike na Serikali kupata mapato yake.

Mruma ameyasema hayo leo Oktoba 30, kwenye Kikao cha tume jijini Dodoma, chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa za utendaji wa Tume kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini Idris Kikula, Makamishna wa Tume, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Yahya Samamba na menejimenti ya Tume ya Madini.

Amesema, kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara kupitia ziara, makongamano, warsha na maonesho mbalimbali sambamba na kuongezeka kwa kasi ya uchakataji wa maombi ya leseni za madini.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo akielezea hali ya utekelezaji kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini amesema, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, mwaka huu kamati yake ilipokea mipango ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini 234 ambapo mipango 232 ilipitishwa baada ya kukidhi vigezo.

Amefafanua kuwa, elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini imeendelea kutolewa sambamba na matumizi ya mfumo wa usimamizi wa ushirikishwaji wa watanzania, katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii kwa wadau wa madini nchini.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Yahya Samamba akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli amesema, kati ya kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, mwaka huu Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 184.53.

Eng. Yahya amesisitiza kuwa Tume kupitia Ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa, imeendelea kuweka mikakati kabambe ili kuhakikisha lengo ililopewa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882.12 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023-2024 linafikiwa.

Katika hatua nyingine, Eng. Samamba ameeleza kuwa katika kipindi husika, ulifanyika ukaguzi wa migodi, mitambo ya uchenjuaji wa madini na utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo mbalimbali nchini hasa kuhusu usalama kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

“Tume ilifanya ukaguzi ili kutathmini eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la topesumu kwenye migodi au mitambo ya uchakataji wa madini katika miradi ya Green Pacific Investment Limited kwenye Kijiji cha Mbangala, Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe.

“Adam Thomas Mungirwa katika Kijiji cha Mtakuja, Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi; Kampuni ya Mwaloni Limited iliyopo Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara; Hexad Company Limited na Nyati Gold Mine katika Mkoa wa Geita na Msalala Gold Mine Ltd iliyopo Kahama, Mkoani Shinyanga,” amesisitiza Eng. Samamba.

Ameongeza kuwa, ulifanyika ukaguzi kwa ajili ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa mabwawa ya topesumu katika miradi ya Lindi Jumbo na Uranex mkoani Lindi, Taur Tanzania Limited katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora na Mgodi ya Peponi Mkoani Singida kwa lengo la kuangalia uzingatiaji wa Sheria ya Madini Sura ya 123 na kanuni zake.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesisitiza umuhimu wa kufuatilia madeni ya leseni za madini ambazo hazijalipiwa na watumishi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Tume.