Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Venance Kasiki amesema kuwa Tume imeendelea kubuni vyanzo vipya vya ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli la shilingi bilioni 650 lililowekwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2021-2022.
Kasiki ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye Kikao cha Tume ya Madini kilichofanyika kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa Tume kwa kipindi cha robo mwaka (Oktoba hadi Desemba, 2021)
Ametaja vyanzo vipya vilivyobuniwa kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa migodi mikubwa ya uzalishaji wa madini ikiwa ni pamoja na mgodi wa uchimbaji wa madini ya nikeli wa Tembo Nickel utakaoendesha shughuli zake katika eneo la Kabanga mkoani Kagera na mgodi wa dhahabu wa Sota Mining Corporation utakaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini hayo katika eneo la Sengerema mkoani Mwanza.
“Leseni za kampuni hizi zilitolewa kati ya kipindi cha mwezi Oktoba na Desemba mwaka 2021 ambapo tunaamini zitaongeza kwa kiasi kikubwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli,” amesisitiza Kasiki.
Ameongeza mikakati mingine ya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na kuongeza usimamizi kwenye shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwanda ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa maduhuli kwa njia ya kielektroniki wa madini hayo.
Ameongeza kuwa Tume imekuwa ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye usimamizi wa biashara ya madini kwenye masoko ya madini pamoja na ukaguzi wa madini ujenzi na ya viwandani yanayosafirishwa kutoka eneo moja kwenya eneo jingine.
Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli, Kasiki amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba mwaka 2021, Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 313 na kusisitiza kuwa siri ya kuendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa maduhuli ni pamoja na uchapakazi na ubunifu wa watumishi wa Tume Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
Katika hatua nyingine ameongeza kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua kutoka asilimia 7.3 mwezi Julai, 2021 hadi 7.9 mwezi Desemba, 2021.
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Lekashingo akielezea utekelezaji wa mpango wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Septemba hadi Desemba, 2021 mipango 158 ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini (Local Content) iliwasilishwa ambapo mipango 156 ilipitishwa huku miwili iliyobaki ikipewa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho.
Amesisitiza kuwa Tume ya Madini imeendelea kutoa elimu kwa kampuni za madini na watoa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kuhusu namna ya uwasilishaji wa maombi ya mipango ili kuridhiwa na kuanza kutoa huduma.
Aidha ameongeza kuwa kutokana na Tume kufanya vizuri kwenye eneo la ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini, hivi karibuni ilikabidhiwa tuzo na Jukwaa la Uwekezaji Tanzania baada ya kuwa mshindi wa pili kwenye kundi la Taasisi za Serikali zinazosimamia eneo hilo.
Naye mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula sambamba na kupongeza mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli na utekelezaji wa majukumu ya Tume, ameelekeza watendaji kuendelea kuchapa kazi kwa ubunifu zaidi ili Sekta ya Madini izidi kukua.
“Pamoja na majukumu mengine, Tume ya Madini imepewa jukumu kubwa la ukusanyaji wa maduhuli ambalo ni kipaumbele kikubwa, ni vyema tukaendelea kuweka rekodi nzuri ya ukusanyaji wa maduhuli, ili fedha zinazotumika zisaidie kuimarisha sekta nyingine,” amesisitiza Profesa Kikula.
Kikao hicho kimeshirikisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Dkt. Faraji Mnyepe, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa, Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Haroun Kinega na Makamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma na Janeth Reuben Lekashingo.
Wengine ni pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Venance Kasiki, Wakurugenzi na Mameneja wa Tume ya Madini.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu