November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tujenge sekta binafsi yenye nidhamu,uwazi- Balozi Kattanga

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ameitaka sekta binafsi kufanya shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya nidhamu, uwajibikaji na uwazi ili kuleta ufanisi zaidi kwa sekta hiyo ambayo ni injini muhimu kwa maendeleo na ukuaji wa uchumi.

Akizungumza kwenye mkutano wa Kamati Tendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ulifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ikiwa sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 12 wa baraza hilo utakaongozwa na mwenyekiti wa baraza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wiki hii, Balozi Kattanga amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuwa na ukaribu zaidi na sekta binafsi.

“Serikali ya awamu ya sita imekuja na mbinu tofuti ambayo ni shirikishi katika kutekeleza miradi yake, tutashughulika na mtu au taasisi yoyote ambayo inafuata misingi ya nidhamu na uwajibikaji,’’ amesema Balozi Kattanga ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya TNBC.

Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga akizungumza katika kikao cha kamati hiyo kinachojumuisha wajumbe kutoka sekta binafsi na uuma ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 12 wa TNBC utakaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan.

Ameitaka sekta binafsi na umma kubadilika kimtazamo na wote kufanya kazi kama timu na pale ambapo changamoto zitakapobainika, vikao vya kamati tendaji ambavyo wajumbe wake hutoka sekta binafsi na umma kukaa na kuja na majawabu ya pamoja.

“Serikali itaendelea kuweka mikakati yake vizuri ya kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji sambamba na kutengeneza ajira kwa vijana, huduma za afya pamoja na elimu,’’ amesema.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Godwill Wanga, amesema mkutano huo umepokea na kujadili mawasilisho matatu ya tafiti ambayo yalihusu kuendeleza viwanda vya misitu, kuboresha usimamizi wa kodi na namna ya kupanua wigo wa walipa kodi pamoja na nafasi za taasisi za udhibiti kusimamia badala ya kuwa washindani.

“Tumepokea mawasilisho matatu ambayo tumeyajadili na kuyapitisha kwa ajili ya kikao cha 12 cha baraza kitakachofanyika tarehe 26 June, 2021 chini ya Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo,’’ amesema.

Ameongezea kuwa wajumbe wa mkutano huo wameonesha matumaini makubwa kwa hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuifanya sekta binafsi inatoa mchango unaostahili kwenye ukuaji wa uchumi na pato la Taifa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema mipango imewekwa kuhakikisha nchi inafikia uchumi wa juu kwa kuweka mazingira rafiki ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga akiongoza kikao cha kamati hiyo kinachojumuisha wajumbe kutoka sekta binafsi na uuma ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 12 wa TNBC utakaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan.

“Tunahitaji kuwa na sekta binafsi yenye nguvu na ndiyo maana Serikali inatekeleza miradi mingi kwa ubia na sekta hiyo na ili kuweka mazingira mazuri zaidi kwenye bajeti ya mwaka 2021/22 tumefuta baadhi ya kodi pamoja na kupunguza tuzo mbalimbali,’’ amesema Tutuba.

Dkt. Jacqueline Mkindi ambaye ni mjumbe wa kamati amesema uwepo wa TNBC kama kiungo muhimu kati ya sekta ya umma na binafsi umesaidia sana katika kutatua changamoto za biashara na uwekezaji hapa nchini.

“Tunaishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuweka pamoja sekta za umma na binafsi ili kutimiza azma ya maendeleo endelevu kwa kuanzisha baraza ambalo limekuwa sehemu ya fursa ya kujadili na kutoa masuluhisho ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabishara na wawekezaji hapa nchini,” amesema.