Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imemteua na kumkabidhi rasmi mwanablogu na mtangazaji wa utalii kutoka Oman, Khalid Hamed Al Barwani, Ubalozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania kwa kutambua mchango wake katika kuitangaza Tanzania kwenye majukwaa ya kimataifa.
Ubalozi huo ulikabidhiwa na Mkurugenzi wa TTB, Ephraim Mafuru, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Al Barwani amepata umaarufu nchini baada ya kuongoza kundi la Dream Team Explorers kutembelea Shamba la Miti Sao Hill mwaka 2024, ambapo walivutiwa na mandhari ya misitu ya kupandwa, mazingira ya asili na vivutio mbalimbali vilivyopo katika eneo hilo.
Kupitia ziara hiyo na machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii, Al Barwani alichangia kuongeza mwonekano wa Sao Hill na vivutio vingine vya Tanzania kwa hadhira ya kimataifa, hatua iliyosaidia kuhamasisha watalii wengi zaidi kuvutiwa na nchi.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi ubalozi huo, Mafuru amesema uteuzi wa Al Barwani unatokana na mchango wake mkubwa katika kuitangaza Tanzania na kwamba mabalozi wa hiari wa utalii wana nafasi muhimu katika kufungua masoko mapya ya utalii duniani.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa kimataifa ili kuimarisha kampeni za kutangaza utalii wa Tanzania na kuongeza ushindani wa nchi katika sekta hiyo.
Uteuzi wa Al Barwani unatarajiwa kuimarisha zaidi juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa, kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya nchi na kuchangia ukuaji wa mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

More Stories
Vodacom yang’ara sabasaba,yatwaa tuzo mbili
Serikali yaongeza kasi Mpango wa Umeme Nyuklia
Misime: Hali ya Usalama ni Shwari, Wananchi waendelee na shughuli zao