Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
SERIKALI imeanza maandalizi ya awali ya kuanzisha uzalishaji wa umeme wa nyuklia, huku ikisisitiza kuwa hatua zote zinazochukuliwa zinafuata viwango vya kimataifa vya usalama ili kulinda afya za wananchi na mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema hayo leo Julai 5,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda hilo katika maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaa.
Amesema, Tanzania ipo katika hatua za awali za maandalizi kabla ya kuanza rasmi utekelezaji wa mpango huo kwa kuzingatia miongozo ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Amesema Serikali kwa sasa inaweka mfumo madhubuti wa sheria, sera na taasisi zitakazosimamia matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kabla ya kuanza uzalishaji wa umeme.
“Tunataka kuhakikisha msingi wa matumizi ya nishati ya nyuklia unakuwa salama na wenye kuzingatia viwango vyote vya kimataifa kabla ya kuanza uzalishaji wa umeme,” amesema Prof. Najat.
Ameeleza kuwa TAEC tayari imewaalika wataalamu wa kimataifa kufanya tathmini ya kiwango cha utayari wa Tanzania, ambapo matokeo yatakayoonyesha nchi imekidhi vigezo yatafungua njia ya kuendelea na hatua zinazofuata za utekelezaji.
Kwa mujibu wa Prof. Najat, Serikali inalenga ndani ya kipindi cha takribani miaka saba kuwa imefikia uwezo wa kuzalisha umeme wa nyuklia ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya uchumi na viwanda.
Kuhusu malighafi, amesema Tanzania ina akiba ya madini ya urani, lakini madini hayo hayawezi kutumika moja kwa moja bila kuchakatwa kwa teknolojia maalumu yenye viwango vya juu.
Amefafanua kuwa katika hatua za mwanzo, urani itachimbwa nchini na kusafirishwa kwenda katika nchi zenye uwezo wa kuichakata kuwa mafuta ya nyuklia, ambayo baadaye yatarudishwa Tanzania kwa matumizi ya kuzalisha umeme.
Aidha, amesema mradi wa kwanza wa uchimbaji wa urani unatarajiwa kuanza katika eneo la Mkuju, mkoani Ruvuma, wakati tafiti za kubaini maeneo mengine yenye akiba ya madini hayo zikiendelea.
Prof. Najat amewataka wananchi kuwa na uelewa sahihi kuhusu teknolojia ya nyuklia na kuondoa hofu zisizo na msingi, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaendelea kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.

More Stories
TTB yamteua khalid al barwani kuwa Balozi wa Utalii
Misime: Hali ya Usalama ni Shwari, Wananchi waendelee na shughuli zao
Mbibo:Boresheni utoaji leseni za Madini kupunguza Migogoro