May 27, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRFA wapata mdhamini mpya wa ligi ya mpira ya Rubi International

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Chama cha soka mkoa wa Tanga ‘TRFA’ kimepata mdhamini mpya wa ligi ya mpira (Rubi International ) kamapuni inayojihusisha na uuzaji na uchimbaji wa madini ambaye ameahidi kuboresha mashindano hayo kila msimu hatua ambayo ni njia moja wapo ya kuongeza ushindani kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya kuibua vipaji vipya kwa vijana kupitia mpira wa miguu watakaokuja kufanya vizuri hapo baadaye kupitia timu za ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Akizungumza na kituo hiki mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Tanga ‘TRFA’ Saidi Sudi alisema hatua ya kumpata mfadhili huyo ni jambo ambalo limeweka historia kwa soka la Tanga ambayo sasa inakwenda kukiinua chama hicho pamoja na kuboresha michuano hiyo huku akiwashukuru na kuona kuwa Tanga ni sehemu salama kwa ajili ya kufanya nao kazi.

“Kwa bahati nzuri katika historia ya chama cha soka mkoa tumepata mfadhili ambaye anakwenda kuboresha ligi yetu ya mkoa kupitia zawadi na mengineyo kwa namna ya pekee tunawashukuru sana kwa kutuona na kutuchagua kuwa Tanga ni mahali pekee ya kufanya udhamini” alisema Sudi.

Mwakilisi wa kampuni ya Rubi International Tom Machupa alisema watazidi kufanya bora zaidi kwaajili ya kukuza vipaji na kuipa hadhi ligi hiyo ambayo kwa namna mmoja ama nyingine sasa inakwenda kuwa ligi bora Tanzania bara kwa ngazi ya mkoa.

“Huu ni mwanzo tu na hayo mengine yatazidi kuboreshwa kwaajili ya ligi ya mkoa wa Tanga, kadiri siku zinavyoendelea tutafanya zaidi na tunaamini ligi hii inakwenda kuwa bora zaidi tofauti na ligi yeyote hapa nchini kwa ngazi ya mkoa”alisema Machupa .

Ligi hiyo ambayo huzishirikisha timu 16 kutoka wilaya zote 8 za mkoa wa Tanga kila msimu, msimu huu itakwenda kutamatishwa hapo kesho January 2, 2022 itakapochezwa fainali ya kumtafuta bingwa mpya wa mkoa ambapo Vijana wa Veterans tayari wameshaingia fainali wakimsubiri kwa hamu atakaye chuana naye kati ya Magomeni United na Pangani City ambao wanacheza nusufainali kutafuta tiketi ya kuingia hatua hiyo.

Kwa msimu huu wa ligi ya mkoa 2021/2022 ambayo inakwenda kutamatishwa hapo kesho kampuni ya Rubi International unayofanya shughuli za madini imetoa zawadi ya vikombe kwa timu itakayochukuwa ubingwa , kocha bora, mchezaji bora , mfungaji bora pamoja na timu yenye nidhamu ambayo itapewa hati ya kutambuliwa kushiriki ligi hiyo.