May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yatoa elimu ya kodi kwa wanaCCM

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Jimbo la Ilala.

Hata hivyo amesema viongozi hao na wanachama hao wanapaswa kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwani bajeti ya serikali ni Sh. Trilioni 44 na kati ya hizo, Trilioni 26 zinatakiwa kutolewa na TRA ambayo ni sawa na asilimia 60.2 ya bajeti yote ya serikali.

Ofisa Msimamizi wa kodi Mkuu kutoka TRA, Hamad Mterry, amesema ni umuhimu kulipa kodi kwani bajeti ya serikali ni Sh. Trilioni 44 na kati ya hizo, Trilioni 26 zinatakiwa kutolewa na TRA ambayo ni sawa na asilimia 60.2 ya bajeti yote ya serikali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 16, 2024 katika semina ya kuwajengea uwezo viongozi na wanachama hao, amesema wameamua kutumia jukwaa hilo kutoa elimu ya mlipa kodi kwani kupitia viongozi hao ambao wapo takribani 90 ujumbe utawafikia watu wengi.

“TRA tuna jukumu zito la kuchangia bajeti ya serikali, hivyo tunawasihi wananchi na wafanyabiashara muwe na moyo wa kulipa kodi kwa hiari,naomba mtoe taarifa za watu wanao kwepa kodi, mtu akifanikiwa kutoa taarifa ataweza kujipatia asilimia tatu ya kodi iliyokombolewa ambayo kiwango cha mwisho ni milioni 20,”ameeleza.

Ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha mwezi Machi TRA imekuwa ikifanya makadirio ya kodi ambayo mtu atalipa mwaka mzima kwa awamu nne tofauti.

Vilevile amesema wameamua kutumia jukwaa hilo kuendeleza kampeni ya kuwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kudai risiti na yule anayehudumia atoe risiti.

“Ni muhimu kudai na kutoa risiti Kwasababu unapofanya hivyo yale mauzo yanakuwa yamerekodiwa kupitia mfumo wetu na hata mfanyabiashara akiyaficha mauzo yake sisi tayari tunakuwa nayo”amesema Mterry.

Awali Mbunge wa Ilala na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amewasihi watanzania kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Amesema lengo kuu la serikali ni kuondoa utegemezi kwa mataifa mengine na kujivunia maendeleo ya nchi kwa kulipa kodi.

“Ni muhimu kulipa kodi…,leo Watanzania tupo milioni 61, hivyo bila kodi na uwekezaji mkubwa hatuwezi kusaidia katika kupata huduma bora,nawaomba viongozi na wanachama wenu hao kutoa somo hilo walilopatiwa sambamba na kuwatahadharisha wafanyabiashara kuwa TRA inajua kila kitu, hata pale wasipotoa risiti wanajua na wakitoa wanajua,”.

Naye Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ilala, Said Sultan amesema viongozi hao wana wajibu wa kuhimiza na kushawishi wananchi kulipa kodi.