May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA Mkoa wa Kilimanjaro kutowavumilia wafanyabiashara wanaokwepa kodi

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi

MAMLAKA ya mapato nchini (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro, imesema haitavumilia wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuinyima serikali mapato yake.

Hata hivyo TRA,imesema itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuhakikisha wanalipa Kodi kwa mujibu wa sheria lakini pande hizo mbili zinakuwa na mahusiano mazuri.

Kaimu meneja wa TRA,Tirson Kabuje alisema hayo katika kikao na wafanyabiashara wa vipuri vya vyombo vya moto na wamiliki wa karakana za vyombo hivyo Mjini Moshi.

Alisema Mamlaka imetimiza wajibu wake wa kuwafuata wafanyabiashara ili kuhakikisha wanafuata sheria bila kutumia nguvu na kuepusha misuguano isiyo wa lazima.

Alisema zipo changamoto ya wafanyabiashara kutotunza kumbukumbu za hesabu, kutotoa risiti wakati wa manunuzi na uuzaji jambo ambalo linaikosesha serikali mapato.

Mapema Ofisa msimamizi wa walipa kodi wa TRA mkoani hapa, Odupoi Papaa,alitaka wafanyabiashara kujenga mahusiano Bora na Mamlaka hiyo ili kupata elimu sahihi kuhusu Kodi badala ya kuendesha biashara kinyume cha sheria.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Papaa alitaka wafanyabiashara kuhakikisha wanapelela taarifa za mwenendo wa biashara kabla ya Tarehe 20 ya kila mwezi, (Returns) bila kujali wamefanya mauzo ama la.

Alisema wafanyabiashara Wana wajibu wa kufanya matumizi sahihi za mashine za kieletroniki (EFD), kujikadiria kodi lakini pia taratibu za kupata vitambulisho vya mjasiriamali.

Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoani hapa, Hilary Lyatuu aliomba TRA kuingilia kati suala la wafanyabiashara kupanga bidhaa za vilainishi vya mashine barabarani badala ya maeneo rasmi.

Katika majibu ya TRA, kuhusu suala Hilo, wafanyabiashara walitakiwa kuwasiliana na halmashauri ya Manispaa ya Moshi ndiyo yenye dhamana ya kupanga wafanyabiashara kulingana na mipango miji.