May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakilishi wa Wakulima katika Kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga mkoani Tabora,akipokea kadi yake ya Matibabu kutoka kkwa Mkuu wa mkoa wa tabora Dkt. Philemon Sengati baada ya uzinduzi wa huduma hiyo wapili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya Bernard Konga na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Sabasaba Moshingi.

TPB, NHIF wazindua mpango bima ya afya kwa wakulima

Na Mwandishi Wetu, Igunga

BENKI ya TPB kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) imezindua huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima kupitia mpango wa Ushirika Afya unaotolewa na NHIF.

Mkuu wa Mkoa Tabora, Dkt. Philemon Sengati alizindua rasmi huduma hiyo mkoani Tabora katika kijiji cha Mwamashimba kilichopo wilaya ya Igunga mwishoni mwa wiki.

Hafla hiyo ilishirikisha wakulima mbalimbali kutoka vyama tofauti katika Mkoa wa Tabora pamoja na uongozi wa Serikali mkoa na wafanyakazi wa Benki ya TPB na NHIF.

Makubaliano ya kuja na huduma hii yaliusisha pande tatu ambazo ni Benki ya TPB, NHIF na vyama vya ushirika katika kanda ya ziwa.

Mpango huu umepangwa kuongeza vyama vingine vya msingi kama, vile Shinyanga Cooperative Union (SHIRECU), KAHAMA COOPERTIVE UNION (KACU), SIMIYU COOPERATIVE UNION (SCU), Nyanza Cooperative Union (NCU) na vyama vingine vilivyopo kanda ya Ziwa.

Vyama vya Msingi vya Ushirika kupitia ofisi ya mrajis wa vyama vya Ushirika nchini vitaingia makubaliano NHIF na Benkiya TPB ambapo watasaini Makubaliano ya Awali (MoU) ya ufanyaji kazi kwa kanda ya ziwa maana ndipo huduma hii itakapopatikana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benkiya TPB, Sabasaba Moshigi alisema;

“Kwa sasa Mpango huu wa Huduma ya Afya kwa wakulima, umeanza na Mazao ya Kimkakati hususani zao la Pamba ambalo linalimwa zaidi kanda ya ziwa”. “Huduma hii ya Bima ya Afya Kwa wakulima imeanza kwama jaribio katika Kanda ya Ziwa ambako zao la pamba linalimwa kwa wingi na majaribio ya huduma hii yanafanyika kwa kushirikiana na chama cha Ushirika cha Igembensabo Cooperative Union kilichopo Igunga-Tabora”, aliongeza Moshingi.

Huduma hii aina makato yoyote na itapatikana katika matawi yote ya benki ya TPB kanda ya ziwa na ofisi za NHIF.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema, “Mkulima kupitia vyama vya msingi atachangia sh. 76,800, mwenza wake atachangia sh. 76,800 na watoto chini ya miaka 18 watachangia sh. 50,400 kwa mwaka”, alisema Konga.

“Makato yatafanyika palemkulima atakapokuwa analipwa fedha ya mazao yake kupitia chama chake cha ushirika,” aliongeza Konga.

Pia vile vile mkulima akishapewa kadi yake ya bima “Bima Afya Kadi” atanufaika na hudumazifuatazo; kumuona daktari, huduma ya dawa, vipimo, wagonjwa wa nje na kulazwa, upasuaji mdogo, mkubwa na wakitaalamu, afya ya kinywa na meno, tiba ya macho, miwani ya kusomea, mazoezi ya tiba ya viungo nk.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Philemon Sengati aliushukuru uongozi wa Benkiya TPB pamoja na NHIF kwa kuja na huduma hii kwa wakulima. Alisema,

“Wakulima ni kundi ambalo kwa namna moja au nyingine lilisahaulika katika upatikanajiwa huduma ya afya nchini, napenda kuishukuru TPB na NHIF kwa kukumbuka kundi hili nchini”. “Napenda kutoa rai kwa taasisi nyingine za serikali ziweze kuiga mfano wa TPB na NHIF katika kukumbuka makundi mbalimbali nchini”.

Naye Menejawa Tawi la TPB mkoani Tabora Bw. Timon Massawe alisema, “Kwa kupitia mpango huu benki yetu itaweza kuongeza wigo wawateja, kufungua akaunti za vyama vya ushirika kwa ajili ya makusanyo ya bima na pia shughuli za uendeshaji wa chama”.