Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Mafuta ya Total, imezindua kituo kipya cha mafuta cha Total Mshingeni kilichopo Goba na imempongeza Rais John Magufuli, na serikali yake ya awamu ya tano kwa kujenga mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji.
Mazingira hayo yametajwa kuiwezesha kampuni ya Total kuendelea kuwekeza nchini na kuahidi kwamba sio tu itaendelea kuwepo nchini ili kufanya biashara ya mafuta, bali itawajengea uwezo Watanzania kwa kuwawezesha na kuwapatia fursa za kuingia katika biashara ya vituo vya mafuta vya kiwango cha kimataifa kama vya Total, kupitia ubia unaitwa DODO.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Jean Schoepp wakati wa uzinduzi wa kituo kipya cha mafuta cha Total, Total Mchigani, kilichopo Goba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kituo hicho kinachomilikiwa na Mtanzania mzawa kikiwa kwenye moja ya barabara yenye shughuli nyingi za kiuchumi jijini Dar es salaam inayotokea Mbezi Beach hadi Mbezi Kimara, hivyo kulenga kuwahudumia wakaazi wa Tegeta, Mbezi Beach na Kimara pamoja na watumiaji wote wa barabara hiyo.
“Napenda kutumia nafasi hii kueleza kuwa Total Tanzania, bado ipo, ilikuwepo, na itaendelea kuwepo,”amesema Schoepp na kuongeza; “Total tunamshukuru Rais Magufuli na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwezesha ukuaji wa kibiashara kwenye sekta ya nishati.
Pia tunatambua kuwa uzinduzi huu usingewezekana pasingekuwa na baraka za Serikali ambayo waliidhinisha leseni za kuendesha kituo hiki na kwa hilo shukrani zangu za dhati zinaenda kwa EWURA na pamoja na taasisi zingine za Serikali zilizowezesha jambo hili kufanikiwa.”
Ameongeza kuwa Total Tanzania imekuwa ikihimiza wamiliki wa biashara kukuza biashara zao kwa kuingia ubia wa kibiashara na kampuni hiyo kwa njia ya DODO ambayo itawawezesha kumiliki na kuendesha vituo vya mafuta vyenye chapa ya Total.
DODO ni mfumo wa kibiashara ambao kampuni ya hiyo hutumia kuweza kuongeza mtandao wa vituo vyake nchini. Mfumo huu unawawezesha wafanyabiahsara kuingia kwenye ubia na kampuni ya Total na kuweza kumiliki, kuendesha Pamoja na kusimamia vituo vya huduma vya Mafuta vyenye chapa ya Total.
Schoepp amesema Total inalenga kumfikia kila Mtanzania na kuwapatia nafasi ya kufuruhia huduma na bidhaa nzuri kutoka Total. “Pia tunawaalika wafanya biashara ambao wangependa kupanua biashara zao kuungana nasi kupitia mpango wetu wa DODO na kupata nafasi ya kumiliki kituo cha huduma ya mafuta na kuweza kupanua na kuimarisha biashara zao,”amesema.
Amengeza kuwa; “Leo (Juzi), tunafurahia kuingia katika ubia wa kibiashara na Mhandisi Frank Malle ambaye ni mmiliki wa kampuni ya F.S Mshuwa Co na mmiliki wa kituo hichi.
Kwa ushirikiano huu tunatarajia kuihudumia Goba na jamii inayoishi maeneo ya jirani. Pia ningependa kutumia fursa hii kuwaalika wafanya biashara ambao wangependa kupanua biashara zao kuungana nasi kupitia mpango wetu wa DODO na kupata nafasi ya kumiliki kituo cha huduma ya mafuta na kuweza kupanua na kuimarisha biashara zao.”
Akizungumza kuhusu Total, Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano wa Total, Marsha Msuya-Kileo, amesema; “Sisi Total haijaja tunapokuja Tanzania, hutuji tu Tanzania kwa ajili ya kuuza tu mafuta na kuondoka, tunakuja Tanzania, tunauza mafuta, na tunahakikisha tunawapa ujuzi wa kujenga vituo vya Total, ujuzi wa kuuza mafuta ya Total, na kuwajengea uwezo wa kumiliki vituo vya Total kwa mfumo wa DODO”.
Marsha anaendelea kueleza; “Hii ni DODO yetu ya 8, Total ina mpango wa kuweka DODO 100, hivyo bado kuna fursa kwa Watanzania 92, wenye maeneo ya pembezoni mwa barabara yanafaa kujengwa vituo vya mafuta, waje Total, wajengewe uwezo, wawe wamiliki wa vituo vya mafuta vya Total kwa mfumo wa Dodo.
Kwa upande wake, mmiliki wa kituo hicho, Malle, ameishukuru Total sio tuu kwa kuwawezesha kumiliki kituo hicho, bali pia kuwaokoa wasiuze ardhi yao, maana walishawishiwa sana kuuza ardhi, lakini Total ikawakomboa, sasa na wao ni wamiliki wa kituo cha kisasa cha mafuta cha Total.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati