January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TNBC yawahimiza Diaspora kuwekeza nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Dar

BARAZA la Taifa la Biashara (TNBC) limewahimiza Watanzania waishio nje ya nchi kuchangamkia fursa za kibiashara na uwekezaji zilizomo nchini sambamba na kuwashawishi wawekezaji wengine kuwekeza Tanzania.

Akizungumza kwenye kipindi maalumu cha Redio Kilimanjaro nchini Marekani juu ya uwekezaji wa Diaspora Tanzania, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga, amewataka Watanzania waishio ughaibuni kuelewa kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yameboreshwa sana na kuwataka waje Tanzania kuwekeza.

“Wakati umefika sasa kwa Watanzania waliopo nje ya nchi kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya biashara na uwekezaji vilivyomo nchini ili Tanzania ipate wawekezaji wengi na nchi ipige hatua kimaendeleo na kiuchumi,” amesema Dkt.Wanga

Amesema kuna fursa za biashara na uwekezaji kwenye sekta za utalii, miundombinu, kilimo na biashara na kuwataka wanadiaspora kuchangamkia fursa hizo na kuwekeza katika sekta hizo ili taifa linufaike na uwekezaji huo.

“Ujenzi wa miradi ya kimkakati ya reli ya kisasa(SGR), Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere ni miradi kwa aina fulani inaohamasisha uwekezaji kwenye hoteli, vituo vya afya na maeneo ya biashara. Uwekezaji katika maeneo hayo kutachochea ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema Dkt.Wanga

Ameeleza kuwa kuna fursa za uwekezaji kwenye miundombinu ya barabara za mwendokasi, uwekezaji kwenye mifumo ya maji na afya, ujenzi wa maeneo ya biashara katika viwanja vya ndege na kuwataka washirikiane na Serikali ili waweze kufanya biashara katika mazingira wezeshi.

Ameeleza pia fursa ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuunganisha simu na vifaa vyake na aina nyingine za viwanda vya elektroniki na kuongeza kuwa fursa hii inatokana na kuwepo kwa soko kubwa la simu za mkononi Tanzania na nchi nyingine za Afrika. “Tunawaomba Watanzania waishio nje kutangaza vivutio yetu ili kusaidia kukuza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi,” amesema Dkt.Wanga

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara(TNBC) Dkt.Godwill Wanga akizungumza katika moja ya mikutano ya baraza juu ya uwekezaji wa Diaspora Tanzania na kuwataka watanzania waishio ughaibuni kuhamasisha uwekezaji na biashara kwani mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yameboreshwa zaidi nchini.

Mwenyekiti wa Tanzania Diaspora Hub (TDH), Nassor Basalama, amesema wanadiaspora wamejipanga kufanya tathimini ya mikakati ya kuwekeza nchini Tanzania.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji jambo ambalo litazidi kutupa nguvu ya kufanya uhamasishaji wa kurudi Tanzania na kuwekeza na hata kuvutia wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini,” alisema Bw.Basalama

Amesema TDH imebeba dhamana ya kuhakikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanarudi kuwekeza nchini ili kukuza uchumi wa nchi na kuzalisha ajira zaidi nchi.

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali kupitiaofisi za balozi zetu ili kuendeleza juhudi za kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania,” ameahidi Basalama

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Francis Nanai, amesema TPSF ndio kiungo kati ya wafanyabiashara na serikali na kuhimiza ushirikianao kati ya wanadiaspora na TPSF ambao amesema utuchochea uwekezaji zaidi nchini na nchi kupata maendeleo.

“Wanadiaspora ni sehemu ya sekta binafsi na tayari TPSF imeandaa utaratibu maalum ambao utawawezesha wenzetu kupata taarifa zote muhimu juu ya biashara na uwekezaji ili kuleta urahisi wa wao kutambua fursa zilizopo na kuja kuwekeza,” amesema Nanai