Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
BARAZA la Taifa la Bashara (TNBC) kupitia kikundi kazi chake cha misitu kimeshakamilisha mkakati wa uendelezaji wa viwanda vya kuhandisi mbao mbadala, ambavyo vitasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya misitu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha 8 cha kikundi hicho kilichofanyisha jijini Dar es salaam jana na kuazimia mkakati huo, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga amesema maazimio ya mkutano wa 12 wa Baraza chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ulielekeza kuandaliwa mkakati wa utekelezaji wa mpango EWP.
“Tuliunda kikosi kazi kilichofanya utafiti ambao umefanikisha uandaaji wa mkakati wa utekelezaji wa mpango wa EWP ili kuanza utekelezaji wake ambao utaleta faida kubwa kwa nchi,” alisema Dkt.Wanga.
Alieleza kuwa sekta ya misitu ina fursa kubwa katika kutengeneza ajira pamoja na kuiletea nchi fedha za kigeni, hivyo kupitia mkakati huu utakukwenda kuibua fursa zilizopo kwa wananchi na kupelekea ajira nyingi kuzalishwa kupitia sekta ya misitu.
“Utekelezaji wa mpango huu ambao utasimiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii utachochea uanzishwaji wa viwanda vingi vya kuhandisi mazao ya misitu, jambo litakalopunguza uagizaji wa mbao mbadala kutoka nje ya nchi,” amesema
Dkt.Wanga meeleza kuwa nchi imekuwa ikipoteza fedha nyingi kwa kuagiza mbao mbadala kutoka nje ya nchi, hivyo kupitia mpango wa EWP utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya misitu kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na hata kuuza nje ya nchi.
“Nchi yetu ina malighafi nyingi kwenye sekta ya misitu kuzalisha mbao mbadala kulinganisha na nchi nyingine za jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kwa kuanza uzalishaji tutajiwekeza uhakika wa soko katika Afrika Mashari na mataifa mengine,” amesema Dkt.Wanga
Aidha Dkt. Wanga amesema Baraza kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii litaendelea kutekeleza maazimio ya yaliyoafikiwa ambayo kwa kiasi kikubwa yapo kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano ijayo ili kuleta matokeo chanya kwenye kuliongezea Taifa kipato pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
“Sisi kama TNBC tumeazimia kutekeleza kwa vitendo maazimio na maagizo ya Serikali ambapo sekta ya misitu ni miongoni mwa sekta zilizoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka mitano ili sekta hii iweze kushiriki kikamilifu kwenye kuliingizia Taifa faida,” amesema Dkt.Wanga
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Misitu, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa amesema serikali ya awamu ya sita imejipanga na itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kuboresha sekta ya misistu nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta zingine kama vile sekta ya viwanda jambo ambalo litailetea tija taifa na kuongeza fursa za ajira nchini.
“Kufanikiwa kufanya maazimio kama hayo kutapelekea kufunguka kwa fursa nyingi kwa taifa letu na sio tu kwenye sekta ya misitu bali hata kwenye sekta zingine pia hivyo ninataka niwahakikishie kuwa serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutekeleza na kusimamia maazimio kama haya ambayo yanalenga kuleta maendeleo chana kwa Taifa,” alisema Dkt.Mwakalukwa
Kukamilika kwa mkakati wa uendelezaji wa viwanda vya Kihandisi vya mbao mbadala zitokanazo na mazao ya misitu ulitokana na maazimio ya Mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara uliofanyika tarehe 26 Juni,2021 Jijini Dar es salaam ambao ulioongozwa na Mwenyekiti wake ambaye Rais Samia Suluhu Hassan.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati