May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA yatoa utabiri wa msimu mmoja wa mvua katika mikoa 14 

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MAMLAKA  ya Hali ya Hewa nchini(TMA), imetoa utabiri wa msimu mmoja wa mvua katika mikoa 14  ambayo inatarajiwa kupata  mvua za chini ya wastani hadi wastani kuanzia mwezi Novemba na kuishia kati ya mwezi Aprili mwaka 2023.

Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Utabiri wa TMA,DK Hamza Kabelwa wakati akitoa  utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka unaoanzia Novemba 2022 hadi Aprili 2023, alisema mikoa hiyo   ni Kigoma,Tabora,Katavi,Singida,Dodoma,Ruvuma na Lindi,Mtwara,Njombe,Rukwa,Songwe,Mbeya,Iringa na kusini mwa  Morogoro .

Ameeleza kuwa kunyesha kwa mvua hizo chini ya wastani  imesababishwa na La Nina ambapo kutakuwa na joto la bahari la  chini ya wastani katika eneo la kati la bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kuwa chini ya wastani 

DK Kabelwa amesema Katika nusu ya kwanza ya msimu kuanzia Novemba mwaka 2022 hadi Januari mwaka 2023 vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza.

“Ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu kuanzia Februari  hadi Aprili mwaka 2023 na mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kunyesha Mei  mwaka 2023 katika maeneo mengi,”amesema DK Kabelwa.

Dk Kabelwa amesema athari zinazotarajiwa kujitokeza  upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo hayo yanayopata mvua hizo na kuathiri ukuaji wa mazao na upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo

Amesema athari zingine zinazotarajiwa kujitokeza kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanajibwa maji kwa matumizi mbalimbali kama vike umwagiliaji na uzalishaji wa nishati.

Amesema Mamlaka zote zinatakiwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu.

“Hali hii inaweza kuathiri uoteshaji na ukuaji wa mazao hususan katika kipindi cha Novemba na Desemba 2022 kutakuwa na ongezeko la bisumbufu vya mazao kama vile mchwa,viwavijeshi ,panya vinatarajiwa kujitokeza katika msimu na kuarhiri mazao ya uzalishaji kwa ujumla pamoja na matukio ya moto yanaweza kujitokeza kutokana na vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa,”amesema Dk Kabelwa.

Amesema wakulima wanatakiwa kupanda mazao na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na zinazostahimi upungufu wa mvua kama vile mihogo,viazi mikunde na mazaobya bustani.

Naye Mtabiri wa Halii ya hewa(TMA) Joyce Makwata amesema matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chini ya wastani.