Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za msimu wa 2026-2027 zinatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, hususan katika nusu ya kwanza ya msimu kuanzia Novemba 2026 hadi Januari 2027.
Mvua hizo zinatarajia kuwa za wastani hadi juu ya wa katika maeneo mbalimbali nchini katika msimu wa Novemba 2026 hadi Aprili 2027, huku ikidai uwezekano wa mafuriko, magonjwa ya mlipuko. uharibifu wa miundombinu.
Akitoa utabiri taarifa ya mwelekeo wa Mvua za Msimu wa Novemba hadi Aprili 2027 wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka,Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a,amesema mwenendo huo wa mvua unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, inayohusishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki.
Amesema katika kipindi hicho, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa kunyesha katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa, pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Dkt. Chang’a amesema mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani.
Kutokana na mwelekeo huo wa mvua, amewashauri wakulima kutumia mbinu na teknolojia bora za kilimo ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza mashambani.
Amesema hatua hizo ni pamoja na kuandaa mifereji ya kupitisha maji, kutumia kilimo cha kontua na kutengeneza matuta ili kuzuia maji kutuama mashambani, kupunguza mmomonyoko wa udongo na kulinda rutuba ya udongo.
Awali, Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Ramadhani Omari, akitoa tathmini ya mvua za msimu uliopita wa 2025/2026 na mifumo ya hali ya hewa, amesema viashiria vya mifumo ya bahari vinaonyesha kuendelea kwa hali ya El Niño, inayohusishwa na joto la bahari kuwa juu ya wastani.
TMA imeendelea kuwasisitiza watumiaji wa taarifa za hali ya hewa, wakiwemo wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, sekta ya usafiri na usafirishaji, mamlaka za maji na sekta ya afya, kufuatilia taarifa rasmi na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta zao.
Hatua hiyo inalenga kuwezesha wadau kupanga shughuli zao mapema na kuchukua tahadhari zinazofaa kulingana na mwelekeo wa hali ya hewa ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

More Stories
Mikopo kausha damu kwa Walimu yamchefua DC-Nkasi
TANESCO kuiwezesha HWTZ kuzalisha Megawati 200 za umeme
Bombo yawatafuta waraibu 436