Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tabora
KAYA 23,773 zenye wanufaika 57,129 mkoani Tabora zinatarajiwa kunufaika na huduma ya Bima ya Afya kwa Wote awamu ya pili baada ya kuzinduliwa kwa zoezi la uandikishaji wanufaika wapya.
Akitoa taarifa kwenye uzinduzi wa tukio hilo katika uwanja wa TBC mjini hapa, Meneja wa Kanda wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt.Raphael Malaba ameeleza kuwa tukio hilo ni fursa muhimu kwa ustawi wa jamii.

Amesema awamu ya kwanza walikadiria kufikia jumla ya kaya 15,870 zenye wakazi 70,145 lakini wakasajili wanufaika 27,046 kutoka kwenye kaya 9,981 ambao ni sawa na asilimia 63 ya walengwa wote katika Mkoa huo.
“Awamu hii, tumelenga kusajili kaya 23,773 zenye wakazi 57,129 ili waweze kunufaika na matibabu mahali popote kwa kipindi cha mwaka mzima pasipo kusumbuliwa na mtu, kwa gharama ya sh.150,000 tu kwa wana familia 6,”amesema.
Dkt.Malaba amesisitiza kuwa ili kufanikisha lengo hilo wamejipanga kutoa elimu na kuongeza hamasa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kunufaika na huduma hiyo.
Akizindua tukio hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Benno Malisa, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt.Gerald Mongela ametaja faida za bima hiyo kuwa ni kupata matibabu ya uhakika na kwa wakati ambayo yatasaidia wananchi kupona haraka, kuzuia maambukizi kwa magonjwa yanayoambukizwa na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Hivyo akatoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo wakati huu kabla ya dirisha kufungwa na kuwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha zoezi hilo linasimamiwa ipasavyo ili kusajili wananchi wengi zaidi.
Awali akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uzinduzi huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mohamed Hamdan amempongeza Rais Samia kwa kutenga bajeti ili kutekelezwa huduma hiyo.
Ameeleza kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza bayana kuwa Bima ya Afya itatolewa kwa wananchi wote hivyo akaomba watoa huduma kutoa elimu sahihi kwa jamii ili wananchi wengi wajisajili na kunufaika mwaka mzima.



More Stories
TMA: El Niño kuathiri mvua za msimu 2026 -2027
Mikopo kausha damu kwa Walimu yamchefua DC-Nkasi
TANESCO kuiwezesha HWTZ kuzalisha Megawati 200 za umeme