May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TLHO lawashika mkono wazee,watoto Mbarali

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbarali

WAZEE wasiojiweza na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wilayani Mbarali mkoani Mbeya wamepatiwa msaada wa mahitaji mbalimbali ya kujikimu na shirika lisilokuwa la kiserikali la The Living Hope Organization(TLHO) ili waweze kuendesha maisha yao .

Akikabidhi misaada hiyo leo kwa wazee na watoto Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kuhudumia wazee ,watoto na watu wanaoishi katika mazingira hatarishi(TLHO)Lucy Mwakibete amesema kuwa wazee waliopatiwa msaada ni 15 na watoto 13 ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Akizungumzia misaada waliokabidhi kwa wazee hao mkurugenzi Mwakibete ametaja misaada iliyotolewa kwa wazee ni Mavazi ,sukari, sabuni , mafuta ya kupaka, chumvi na viberiti na kwa upande wa watoto wa shule wamepatiwa sare za shule, sabuni, chumvi pamoja na mafuta ya kupaa na mahitaji mengine muhimu ya shule.

“Lengo la kutoa misaada kwa wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni baada ya kugundua kuwa katika wilaya hiyo kuna wazee wengi wanapitia changamoto kubwa na kugusa mahitaji ya msingi na baadhi walio wengi wametelekezwa na familia zao na kuachiwa mzigo mkubwa wa kulea wajukuu”amesema Mkurugenzi Mwakibete.

Aidha Mwakibete amesema kuwa shirika hilo limeanzisha utaratibu kwa wazee kujiwekea akiba na kukopeshana na kuwa wamelenga zaidi kwa wilaya ya mbarali sababu wakazi wengi wa Mbarali ni wakulima na kwamba vikundi hivyo vina utaratibu wa kuweka hisa na wanakutana kwa wiki mara moja na kununua hisa thamani ya hisa inapangwa kulingana na uchumi wa eneo husika.

Amesema uwekekaji akiba huo unawasaidia kushughulikia masuala ya kilimo na uwekeaji akiba huo unamsaidia mkulima kumpunguzia kutegemea fedha za watu wengine na kufundishwa umuhimu wa kutumia fedha zao wenyewe na kama shirika hawatoi fedha yeyote zaidi ya kuwasaidia vitabu vya kuwekea hisa na masanduku ya kutunzia fedha imekuwa msaada mkubwa kwani hata halmashauri inavitambua vikundi vyote kwani tayari vina usajiri.

Akishukuru misaada hiyo Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Mbarali , Kanali Denis Mwila ameshukuru shirika hilo kwa jitihada kubwa za kuwasaidia wazee wasiojiweza na watoto wanaoishi katika hatarishi na watu wasiojiweza wilayani humo .

“Ni shirika ambalo kwa wilaya ya mbarali mmekuwa mfano mkubwa kwani kazi ya kupita kuomba kwa watu ili kupata mahitaji haya ni kubwa inahitaji uvumilivu nyinyi wenyewe mnafahamu kazi ya kuomba ilivyo ngumu , niombe taasisi na mashirika mengine kulipa ushirikiano shirika hili lakini hata wao kusapoti juhudi zinazofanywa na shirika hili katika kusaidia makundi haya mawili ya wazee wasiojiweza na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi”amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali na Diwani wa kata ya Itamboleo , Twalibu Lubandamo amesema kuwa ameona mabango mbali mbali ya wazee yakisema wazee ni dawa wengi wanaweza wasijue kwanini wazee ni dawa nimeona migogoro mingi vijana wanaharibiana vijana kwa vijana kwa maana vijana wakiulizana changamoto hawawezi kupata majibu sababu akili zinafanana na umri .

Hata hivyo Mwenyekiti huyo amewataka vijana kupitia maadhimisho hayo vijana wanatakiwa wajifunze wanaposema wazee ni dawa wanapokuwa na jambo wakienda kwa wazee wanatibu na ukitoka hapo unapona kabisa.