June 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TISEZA Songea kuvutia uwekezaji, ajira zaidi zapatikana


Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma


MBUNGE wa Songea Mjini, Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, ameibua bungeni suala la mpango wa Serikali kuendeleza Eneo Maalum la Kiuchumi la TISEZA (EPZA Mwenge-Mshindo) lililopo Songea, huku Serikali ikieleza kuwa eneo hilo tayari limevutia wawekezaji wawili wakubwa wanaotarajiwa kuwekeza zaidi ya Shilingi trilioni 2.6 na kuzalisha ajira zaidi ya 6,000.


Akijibu swali la mbunge huyo bungeni jijini Dodoma leo Juni 23,2026, Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji,Dkt. Pius Chaya, amesema Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) imefanikiwa kuvutia wawekezaji hao katika eneo la ekari 4,777.325 lililotengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji na maendeleo ya viwanda.

Katika swali lake Dkt.Ndumbaro alitaka mpango wa Serikali wa kuendeleza eneo la TISEZA (EPZA Mwenge -Mshindo Songea ).


Dkt. Chaya amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuharakisha maendeleo ya viwanda, kuongeza ajira kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla.


Amemtaja mwekezaji wa kwanza kuwa ni Kampuni ya Fazenda kutoka Brazil, ambayo inatarajia kuwekeza katika eneo la ekari 3,012 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 5.2, sawa na takribani Shilingi bilioni 13.52.


Kwa mujibu wa Dkt. Chaya, mradi huo unatarajiwa kutoa ajira 1,200 pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia shughuli za uzalishaji na usindikaji, hatua itakayowanufaisha wakulima kwa kuongeza kipato na kukuza sekta ya kilimo.


Aidha, amesema mwekezaji wa pili ni Kampuni ya HWTZ kutoka China, ambayo imepanga kujenga kiwanda kikubwa cha chuma katika eneo la ekari 1,020 kwa uwekezaji unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni moja, sawa na Shilingi trilioni 2.6.


“Mradi huu unatarajiwa kuzalisha ajira 5,000 na kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya viwanda nchini kwa kuvutia uwekezaji zaidi, kuimarisha minyororo ya thamani ya uzalishaji na kuboresha miundombinu pamoja na huduma za kijamii,” amesema Dkt. Chaya.


Katika hatua nyingine, Serikali imeeleza kuwa ekari 700 zilizobaki katika eneo hilo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya vijana, ujenzi wa ofisi za TISEZA, hospitali ya kuhudumia wananchi na wafanyakazi pamoja na viwanda vingine mbalimbali.


Dkt. Chaya amesema TISEZA inaendelea kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutumia fursa zilizopo katika eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa wananchi.