



Na Mwandishi Wetu ,Dodoma
SERIKALI imesema imejipanga kikamilifu kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na hali ya El Niño kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Akizungumza hii leo 24 Juni, 2026 wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wa usimamizi wa maafa, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Operesheni na Uratibu kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Kanali Selestine Masalamado, amesema kuwa tayari Serikali imeandaa Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura ili kuimarisha maandalizi na hatua za kukabiliana na hali hiyo.
Amesema mpango huo unalenga kuhakikisha kunakuwa na uratibu madhubuti, utekelezaji wa hatua za mapema pamoja na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa wananchi, mali zao na miundombinu.
“Kikao hiki kinatoa fursa kwa wizara, taasisi, mikoa na wadau wengine kupitia rasimu hii kwa kina na kutoa maoni yatakayosaidia kupatikana kwa mpango shirikishi na unaotekelezeka,” amesema Kanali Masalamado
Ameongeza kuwa Serikali inathamini mchango wa wadau wote katika kuboresha mpango huo ili uwe mwongozo thabiti wa kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El Niño.
Aidha, amewataka washiriki kushiriki kikamilifu katika majadiliano na kutoa mapendekezo yenye kujenga yatakayosaidia kulinda maisha ya wananchi na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa hata wakati wa majanga.
Katika hatua za maandalizi, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu tahadhari za kuchukua, ikiwemo kuhama katika maeneo hatarishi na kuendelea na shughuli za kiuchumi katika maeneo salama.
Kwa mujibu wa Kanali Masalamado, kuna umuhimu wa kubaini maeneo salama kwa ajili ya makazi ya muda, pamoja na kuainisha maeneo hatarishi ili kuwezesha hatua za haraka za kukabiliana na maafa.
Sambamba na hilo, amesisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya mawasiliano na utoaji wa tahadhari za mapema ili wananchi wapate taarifa sahihi kwa wakati.
“Ninazikumbusha mamlaka za mikoa na serikali za mitaa kuhakikisha kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi zote zinatekeleza majukumu yao kikamilifu, huku ufuatiliaji ukiendelea kufanyika mara kwa mara,” amesisitiza
Ameongeza kuwa ni wajibu wa taasisi na mikoa kuhuisha au kuandaa mipango yao ya dharura kwa haraka ili Taifa liwe tayari kukabiliana na athari za El Niño endapo zitajitokeza.

More Stories
Serikali kuendelea kupanua fursa elimu Singida
Kumekucha CDF Cup 2026, NMB yaweka Sh milioni 150
TISEZA Songea kuvutia uwekezaji, ajira zaidi zapatikana