Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Dar es Salaam
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),umeipongeza Serikali kwa kushiriki mchakato wa Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) na ushirikiano mkubwa baina yake na asasi za kiraia na Watetezi wa haki za binadamu kabla na wakati wa mapitio ya tatu.
Akizungumza juzi Mjini Geneva,Mratibu wa Kitaifa, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC),Wakili Onesmo Olengurumwa wakati wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa- Kikao cha Kawaida cha 49 suala la 6: Matokeo ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema tayari wameendelea kufanya kazi pamoja na serikali katika ufuatiliaji wa mapendekezo 187 yaliyokubaliwa.
Amesema wanaisihi Serikali kuangalia upya msimamo wake kuhusu mapendekezo 67 ambayo hayakukubaliwa hadi sasa.” Tunashukuru na kutambua maendeleo ya haki za binadamu tunayoendelea kuyapata tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka mmoja uliopita, pamoja na dhamira yake njema na ya Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, katika kukuza, kuendeleza na kulinda haki za binadamu na demokrasia Tanzania Bara na Visiwani,”amesema
Ametoa wito kwa serikali zote mbili chini ya Rais Samia na Mwinyi kuendeleza mapenzi hayo na kupanua dhamira njema katika maeneo mengine yahusuyo haki za binadamu na utawala wa kisheria.
Aidha amesema mtandao wao unatoa wito wa maboresho mapana ya mifumo ya kisheria, ikiwemo ukamilishwaji wa mchakato wa kutengeneza katiba mpya.” Hili linajumuisha pia usimamizi wa mabadiliko ya vifungu vya sheria vinavyoathiri shughuli za asasi za kiraia na Watetezi wa haki za binadamu hususani Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, Sheria ya Vyama vya Siasa, Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (kuhusu Maudhui ya Mtandaoni), Mabadiliko ya Sheria ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, pamoja na Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu na Haki za Msingi za Binadamu (BRADEA),”alisema
Olengurumwa amesema kuwepo kwa mabadiliko ya haraka ya Kifungu cha 4 cha BRADEA ambacho kinazuia asasi za kiraia,Watetezi wa haki za binadamu na watu wenye nia njema kufungua mashauri ya kikatiba kwa lengo la kulinda katiba na kwa niaba ya wahanga wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo makundi maalumu.
“Kifungu hiki kinazuia wajibu wao wa kutetea na kulinda katiba na haki za binadamu kupitia mahakama vilevile, pawepo na jitihada zaidi katika kuhakikisha ongezeko la makosa yanayostahili dhamana na kuacha maamuzi kuhusu dhamana yabaki kwa mahakama,”amesema na kuongeza
“Tunaishauri serikali kwa msisitizo mkubwa isitishe mpango uliopo wa kuwaondoa jamii asili ya wamaasai 70,000 kwenye ardhi yao ya asili iliyoko Tarafa ya Ngorongoro, pamoja na mpango wa kumega ardhi ya vijiji vya Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 Wilayani Ngorongoro,”amesisitiza
Olengurumwa amesema wanasisitiza uwepo wa ushirikishwaji mpana wa jamii unaozingatia misingi ya haki za binadamu katika mipango yote ya serikali ihusuyo maeneo hayo yenye mgogoro Wilayani Ngorongoro.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best