May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEMESA yapongezwa kwa kuwapatia mafunzo watumishi 43 wa vivuko

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) Mhe.Ludovick Nduhiye amewapongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuona umuhimu wa kutenga fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kuwapatia mafunzo watumishi 43 wa vivuko wanavyovisimamia.

Ametoa pongezi hizo Desemba 22,2022 Jijini Dar es Salaam wakati wa Uzunduzi wa Mafunzo kwa Watumishi 43 Wa Vivuko Vinavyosimamiwa na TEMESA Katika Chuo Cha Bahari Dar es Salaam (DMI).

Amesema kupitia mafunzo hayo matarajio ni kuona maboresho makubwa katika uendeshaji wa vivuko vyetu nchini hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini katika kupokea mafunzo watakayopata na kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo na hivyo kuboresha huduma za vivuko nchini.

“Katika kushiriki Mafunzo haya kulingana na fani zenu mnapaswa kutambua kuwa mnalo jukumu la kujifunza kwa bidii ili kuongeza kiwango cha uelewa wenu na hivyo kuboresha utendaji kazi katika maeneo yenu”. Amesema

Aidha amekipongeza Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa kuendelea kutoa mafunzo stahiki kwa watalaam katika kada mbalimbali zinazohusiana na sekta ya bahari na kufanya nchi yetu kuzidi kuzarisha wataalam wanaotoa huduma katika maeneo mbalimabali.

Pamoja na hayo ameielekeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuendelea kufanya ukaguzi wa vyombo vya majini ipasavyo na kuhakiki usalama wa vyombo husika vinavyotumika kusafirisha abiria na mizigo yao vinakidhi vigezo vya usalama na vinaendeshwa na wataalam wenye sifa kulingana na matakwa ya sheria ya vyombo vya usafiri majini.

Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Lazaro Kilahala amesema TEMESA ina jumla ya vituo 22 vyene jumla ya vivuko 33 kote nchini. Kila kivuko kinapaswa kuwa na manahodha, mabaharia, wahandisi pamoja na mafundi wenye sifa zinazoendana na sheria zinazoongoza vyombo vya majini.

Amesema kuwa Wakala utaendelea kutoa mafunzo hayo muhimu kadri ya mahitaji ili kuhakikisha vivuko vyetu vinahudumiwa na watumishi wenye sifa stahiki ili kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

“Kwa kutambua jitihada kubwa zilizofanywa na serikali katika kuhakikisha kuwa fedha kwa ajili ya mafunzo haya zinapatikana tumeona ni muhimu leo tuungane na Serikali katika kuutambua mchango mkubwa katika kufanikisha mafunzo haya”. Amesema