January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCCIA yaja kivingine baada ya kumpata mtendaji mpya

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

CHEMBA ya Wafanyabiashara wenye Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) imepata Mkurugenzi Mtendaji wake mpya ambaye pamoja na mambo mengine ameahidi kuifanyia marekebisho taasisi hiyo sambamba na kuwaleta pamoja wadau wote wa sekta hizo.

Akizungumza mara baada ya kutambulishwa kwa wafanyakazi na Rais wa TCCIA, Paul Koyi, Judith Karangi ameihakikishia Bodi ya Wakurugenzi na wafanyakazi kuwa atafanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ikiwemo kurejesha imani kwa wafanyabiara wote hapa nchini.

“Kwa dhati kabisa ninapenda kuwahakishia nitatekeleza majukumu yangu kwa ufanisi ili sisi kama taasisi muhimu ya kuwaunganisha na kuwasaidia wafanyabishara tunatekeleza wajibu wetu kwa weledi,” amesema Karangi.

Sambamba na hilo, Mkurugenzi Mtendaji huyo mpya amezungumzia pia nafasi ya TCCIA katika kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025 na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na taasisi za Serikali.

Rais wa Chemba ya wafanyabiashara, Biashara, viwanda na kilimo(TCCIA), Paul Koyi (katikati) akimtambulisha Mkurugenzi Mtendaji mpya wa TCCIA, Judith Karangi (kulia) kwenye kikao cha menejimenti na kuwataka watendaji kutoa ushirikiano ili kufikia malengo yaliyoazimiwa. Kushoto ni mjumbe wa Bodi ya TCCIA, Dkt. Said Kingu.

“Nina uhakika tupo vizuri kwa kushirikiana na wadau wote tutaifikisha Tanzania mahali pazuri,” amesema na kuomba ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi, menejimenti, Bodi ya Wakurugenzi na wadau wengine wote.

Awali, akimtambulisha Mkurugenzi Mtendaji huyo mpya, Koyi ameelezea imani kubwa aliyonayo pamoja na Bodi ya Wakurugenzi kwa mkurugenzi mtendaji mpya kwani ataipaisha TCCIA kutoka ilipo sasa na kusonga mbele zaidi.

“Imani niliyonayo na bodi pia kwa mtendaji wetu mpya ni kubwa na matumaini yetu yanakwenda mbali zaidi kuona kwamba kwa uzoefu alionao utakuwa chachu ya kufikia malengo ambayo taasisi imejiwekea,” amesema Koyi.

Aidha Rais huyo wa TCCIA aliwahimiza wafanyakazi wa taasisi hiyo kumpa ushirikiano mkurugenzi mtendaji huyo na kueleza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo yatategemeana na umoja na ushirikiano kwenye utendaji wa kazi.

“Siku zote tunahimizwa “umoja ni nguvu utendano ni udhaifu”, Hivyo basi ninawaomba wafanyakazi wote kumpa ushirikiano wa kutosha mkurugezi mtendaji wetu ili tuweze kufikia malengo mazuri tuliyojiwekea,” amesema.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya TCCIA, Dkt. Saidi Mtemi Kingu amewataka wadau wa sekta za biashara, viwanda na kilimo kumpa ushirikiano mkurugenzi mtendaji huyo mpya kwa kuwa amekuwa mtu mwenye uzoefu kwenye kazi.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Chemba ya wafanyabiashara, Biashara, viwanda na kilimo (TCCIA), Judith Karangi (kulia),akizungumza mara baada ya kutambulishwa na Rais wa chemba hiyo Bw.Paul Koyi (katikati) ) kwenye kikao cha menejimenti na kuahidi kufanya kazi kwa ufanisi ili kuiletea nchi maendeleo.Kushoto ni mjumbe wa Bodi ya TCCIA Dkt. Said Mtemi Kingu.

“Mimi ninapenda niwaondolee hofu wafanyabiashara wote nchini, na wawe na imani kuwa taasisi imepata mtendaji mwenye weledi mkubwa na atakayeweza kusukuma kurudumu la maendeleo na kutimiza matarajio yao,” amesema Dkt Kingu.

Dkt Kingu aliongeza kuwa taasisi hiyo ina nafasi kubwa katika kushiriki kwenye kufanikisha azma ya Serikali ya kuimarisha uchumi na kuwataka watumishi wa taasisi hiyo kumpa ushirikiano mtendaji huyo.

“Sisi kama TCCIA tuna nafasi kubwa kushiriki kwenye kujenga na kuimiarisha uchumi wa nchi yetu, lakini haya yatafikiwa endapo sisi wenyewe kama viongozi tukitekeleza wajibu wetu kwa kushirikiana na uongozi uliopo,” amesisitiza Dkt. Kingu.