May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS yaendesha ukaguzi sokani yakamata vipodozi sampuli 620

Na Angela Mazula

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limefanya ukaguzi wa kushtukiza na kukamata sampuli mbalimbali 620 za vipodozi, huku likiahidi kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa watumiaji wa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje ili kuhakikisha zinakidhi ubora ili kulinda afya za watumiaji.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki Mkaguzi Mwandamizi wa TBS, Mhandisi Donald Manyama alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati maofisi wa shirika hilo walipofanya ukaguzi kwenye maduka makubwa (Supermarket) yaliyopo maeneo ya Barabara ya Bibi Titi yakijihusisha na uuzaji wa vipodozi.

Alisema elimu kubwa inahitajika kwa waingizaji na wasambazaji bidhaa mbalimbali ikiwemo vipodozi.

Kwa mujibu wa Manyama, kwenye ukaguzi huo waligundua baadhi ya maduka yakiuza vipodozi vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 10 vikiwa vimeisha muda wake wa matumizi vingine vikiwa havionesha ni lini muda wake wa utumiaji na havikuwa vikionesha vilitengenezwa lini.

“Maduka haya yamegundulika kuwa na bidhaa ambazo zimepita muda wake. Miongoni mwa bidhaa hizo ni vipodozi kama vile mafuta ya aina mbalimbali ya nywele, mafuta ya kupaka na mengine,” alisema. Mhandisi Manyama.

Aliwataka wamiliki hao waliokutwa wakiuza bidhaa hizo kufika ofisi za TBS ndani ya siku 14 kuanzia sasa ili kuhakiki na kuthibitisha kwamba hicho walichokiona kwenye ukaguzi wao kina ukweli kiasi gani.

Alisema wanatakiwa waeleze sababu za wao kuendelea kuuza bidhaa ambazo hazina muda wa mwisho wa matumizi wala muda kutengenezwa kwa bidhaa hizo, lakini wauza kama wauzaji wameendelea kuziweka sokoni.

Kwa upande wa adhabu kwa walikutwa wakiuza vipodozi hivyo, Manyama alisema kwa wasambazaji faini ni sh. milioni 20 kama atabainika kuwa na kosa na kama wakiendelea tena kufanya kosa ndipo watafikishwa mahakani.

Mmoja wa wafanyabiashara ambaye duka lake lilikutwa likiuza bidhaa hizo, Abdilah Nur alisema hilo sio kosa lao kwa sababu ni jukumu la wasambazaji kujua bidhaaa zenye ubora.

“Kama tukifunga biashara hii watu wangapi watakosa ajira, kwani kuna zaidi ya Watanzania 85 wapo kwenye ajira katika maduka haya.

Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba vitu vinavyouzwa hapa nchini viko katika ubora uliothibitika hapa nchini,”alisema Nur.

Mfanyakazi mwingine akizungumza kwa sharti la jina lake kutotajwa gazetini, alisema hilo ni kosa la kiutendaji kwa baadhi ya idara kukosa weledi wa kutosha na kuruhusu bidhaa zisizokuwa na ubora kuingia hapa nchini.

“Kama kuna uwezekana sheria iongezewe meno kwa yule atayebainika ameruhusu huo uhalifu kutokea ili iwe fundisho kwa wengine. Hii itasaidia na kujenga Tanzania yenye bidhaa zenye ubora kimataifa na kuimarisha zaidi mifumo ili iwe rahisi kumpata aliyeruhusu kutendeka kwa uhalifu huo,” alisema.