Na Penina Malundo,TimesMajira
TANZANIA imejipatia nafasi ya kuwa kitovu cha kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma za kifedha kupitia vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), baada ya kufanikiwa kuwa mwenyeji wa kongamano la Afrika linalowakutanisha wadau zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya nchi.
Kongamano hilo ni fursa kwa Tanzania kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi na uendelezaji wa vyama vya ushirika, huku likitoa nafasi kwa washiriki kujadili mikakati ya kuongeza ufanisi wa SACCOS na kuhakikisha wanachama wananufaika zaidi na huduma za kifedha.
Akizungumza kuhusu kongamano hilo,leo Jijini Dar es Salaam,Wakati wa Kongamano ya 26 la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA) ,Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) iliyochini ya Wizara ya Kilimo,Collins Nyakunga alisema mafanikio ya sekta ya ushirika nchini yametokana na usimamizi wa vyama hivyo pamoja na mazingira yanayowezeshwa na Serikali ili kuimarisha utendaji wake.
Amesema TCDC, iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza vyama vya ushirika nchini, kuhakikisha vinafuata taratibu zilizowekwa na kujenga imani kwa wanachama wanaotegemea huduma zake.

Ameeleza kuwa sekta ya ushirika nchini inahusisha shughuli mbalimbali, zikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na huduma za kifedha kupitia SACCOS, ambazo zimekuwa na mchango katika kuwasaidia wanachama kupata huduma za akiba na mikopo.
Kwa mujibu wa Mrajisi ngamano hilo linalosimamiwa na Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Afrika (COSCA) linatoa nafasi ya kujifunza mbinu bora kutoka nchi mbalimbali, kubadilishana uzoefu na kutafuta njia za kuongeza manufaa ya vyama hivyo kwa wanachama.

Amesema miongoni mwa masuala muhimu yatakayojadiliwa ni namna ya kuhakikisha mikopo inayotolewa kupitia SACCOS inawasaidia wanachama kuboresha hali zao za kiuchumi, pamoja na kuweka mifumo itakayovutia watu wengi zaidi kujiunga na vyama hivyo.
Ameongeza kuwa kongamano hilo limepangwa kufanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 16, mwaka huu, huku ufunguzi rasmi ukitarajiwa kufanyika Oktoba 15 na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waandaaji.

Amesema Tanzania itaendelea kutumia fursa hiyo kujifunza uzoefu wa nchi nyingine, kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuboresha huduma za SACCOS ili ziendelee kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Â

More Stories
NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji.
Familia zatakiwa kuwa na mpango wa kukabiliana na maafa
Mbozi kuibadili stendi ya Malori kuwa Kariakoo.