Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SERIKALI ya Tanzania imetaja vipaumbele sita vinavyopaswa kupewa kipaumbele na Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili bahari na mazingira ya pwani katika miaka ijayo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC),jijini Dar-es-Salaam Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi, aliyemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema vipaumbele hivyo vinapaswa kutafsiri ahadi za mkataba kuwa sheria,taasisi, bajeti na hatua zinazotekelezeka.

Akitaja vipaumbele hivyo ni pamoja na kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi, itifaki zake na maamuzi ya mikutano ya nchi wanachama kupitia sheria za kitaifa, taasisi zenye uwezo, bajeti na mifumo ya utoaji taarifa unaopimika.
Amesema kipaumbele cha pili ni kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kurejesha mikoko, nyasi za baharini na miamba ya matumbawe, kukabiliana na ongezeko la tindikali baharini na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa jamii za pwani zilizo hatarini.
Pia amesema kipaumbele cha tatu ni kuongeza juhudi za kupambana na uchafuzi wa bahari unaosababishwa na plastiki, kemikali na maji taka, huku nchi wanachama zikiboresha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na matukio makubwa ya uchafuzi wa bahari.
Amesema hilo linahitaji mbinu kutoka chanzo hadi baharini, uchumi mzunguko kwa plastiki, kemikali na maji taka pamoja na maandalizi ya kikanda katika kukabiliana na matukio makubwa ya kibahari,na kipaumbele cha nne ni kulinda bioanuwai huku uwekezaji wa baharini ukifanyika kwa uwajibikaji.
Hata hivyo amesema,mipango ya anga ya bahari, tathmini ya mfumo wa ikolojia na hifadhi inayozingatia maeneo inapaswa kuongoza maamuzi kuhusu uvuvi, bandari, utalii, nishati na matumizi mengine ya bahari. Alisema kipaumbele cha tano ni kuwekeza katika sayansi, kushiriki data na kuwa na fedha endelevu.
Kipaumbele cha sita ni kushirikisha sekta binafsi, wanawake na vijana katika juhudi za kulinda mazingira ya bahari na kuendeleza uchumi wa buluu.
“COP12 imeweza kutambulisha kwa mara ya kwanza Jukwaa la Biashara, Jukwaa la Vijana na Ushiriki wa Wanawake, akisisitiza kuwa hatua hiyo inapaswa kuwa kawaida katika mikutano ijayo”amesema.

Ndejembi amesema utekelezaji wa afua mbalimbali lazima uwe jumuishi, huku jamii za maeneo ya pwani, wanawake na vijana wakiwa na sauti katika maamuzi na sehemu ya haki ya fursa za uchumi wa buluu.Huku Tanzania inatambua umuhimu wa kulinda mazingira ya bahari huku ikiendeleza fursa za uchumi wa buluu.
Amesema Bahari ya Hindi ya Magharibi ina thamani ya zaidi ya dola bilioni 300 katika rasilimali, ikizalisha takribani dola bilioni 20.8 kila mwaka, huku mfumo wake wa ikolojia ukiwa na huduma zenye thamani ya dola bilioni 25 kwa mwaka huku zaidi ya watu milioni 65 wanategemea bahari moja kwa moja kwa chakula na riziki zao.
Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni amesema,kupitia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, nchi inalenga kufungua fursa kamili za uchumi wa buluu kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani, kuongeza thamani, uvumbuzi, uwekezaji na kujenga mnyororo imara wa thamani.
Amesema Tanzania inatambua uchumi wa buluu kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu yenye uwezo wa kusaidia uwekezaji, ajira, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi unaoshirikisha wote.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Elizabeth Mrema,amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kutumia jukwaa hilo kugeuza ahadi za kimataifa kuhusu mazingira kuwa hatua zinazotekelezeka katika Bahari ya Hindi ya Magharibi.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa viumbe hai na uchafuzi wa mazingira, ambazo zinahitaji ushirikiano wa nchi kwa kuwa haziwezi kutatuliwa na taifa moja.



More Stories
Ndejembi ataja vipaumbele sita mkutano wa COP 12
Chongolo:Bei ya pembejeo isiumize wakulima
TADB Kanda ya Ziwa kinara katika miradi ya Kilimo