October 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo:Bei ya pembejeo isiumize wakulima

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tabora

WAZIRI wa Kilimo Daniel Chongolo ameeleza kuwa malalamiko ya wakulima wa tumbaku ya kuuziwa pembejeo kwa bei ya juu ikilinganishwa na bei halisi ya zao hilo inapaswa kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili isiwaumize.

Chongolo ametoa kauli hiyo alipokuwa akiongea na viongozi wa ushirika,wadau wa kilimo na wakulima wa tumbaku kutoka Wilaya za Sikonge, Uyui, Nzega na Halmshauri ya Manispaa ya Tabora katika ukumbi wa Themi Hill Sekondari mjini hapa.

Ameeleza kuwa dhamana aliyopewa ni kuhakikisha changamoto zozote zinazogusa maisha ya wakulima zinatatuliwa haraka iwezekanavyo,ambapo msimu uliopita wakulima wengi waliuza kwa bei ya hasara hali iliosababisha sintofahamu miongoni mwao.

“Najua, mbolea za pembejeo zimeshaanza kusambazwa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya msimu mpya, ila nimeambiwa bei bado ni ile ile, nataka ipungue ili isimuumize mkulima, Bodi ya Tumbaku na TCJE lifanyieni kazi,”ameeleza.

Hata hivyo amesema,mikataba ya ununuzi na uuzaji wa zao hilo nayo haiko wazi, haielezi jinsi pande zote zinavyoweza kuwajibika punde mmoja anapoenda kinyume na mkataba wake, na kudokeza kuwa anataka haki itendeke.

“Nataka mikataba yote ya ununuzi wa zao hili iwe wazi na ilinde haki ya pande zote mbili, kinyume na hapo mkulima ataendelea kuibiwa haki yake, na mimi siko tayari kuona mkulima anaonewa, haki na wajibu vinaenda sambamba,”.

Kuhusu madeni ya wakulima, Waziri huyo ameeleza kuwa tayari walishakubaliana, kila kampuni kulipa fedha za wakulima kabla msimu mpya haujaanza, na kuonya kuwa hakuna mnunuzi anayedaiwa atakayeruhusiwa kununua msimu huu.

Aidha amebainisha kuwa yupo tayari kutenga bajeti kwa ajili ya kueneza teknolojia mpya ya ukaushaji tumbaku itakayoleta tija kwenye kilimo cha zao hilo huku akisisitiza kuwa kupanda mti sio mbadala wa kukata mti, bali kulinda na kuhifadhi misitu.

Waziri Chongolo ameonya Maofisa wa Wizara hiyo na Watendaji wa Bodi ya Tumbaku wanaotumia lugha zisizofaa kwa wakulima pale wanapolalamikiwa kutotatua kero zao, huku akiahidi kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kwenda kinyume.