Na Penina Malundo,Timesmajira
TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 30 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Vyuo vya Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Duniani (Association of International Peacekeeping Training Centres -IAPTC ) unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Katika Mkutano huo zaidi ya mataifa 50 yanatarajiwa kushiriki ukiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha na kuleta ubunifu katika operesheni za ulinzi wa amani duniani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati akifungua kikao cha maandalizi ya mkutano huo cha Kamati Tendaji ya IAPTC, Mwenyekiti wa kikao hicho kutoka Italia, Brigedia Jenerali Andrea Paris amesema kwa kawaida mkutano huo hukutanisha kati ya mataifa 50 hadi 60, huku jumuiya hiyo kwa ujumla ikiwa na wanachama kutoka takribani mataifa 90 duniani.
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kutathmini kazi za mwaka mzima za chama hicho na kubaini njia mpya za kuimarisha operesheni za ulinzi wa amani.

“Mkutano huu utatupa Mwanga wa kuangalia changamoto zinazozikabili baadhi ya vituo vya mafunzo ya ulinzi wa amani, ikiwemo uhaba wa rasilimali watu na vifaa, pamoja na kuangalia namna ya vituo hivyo vinavyoweza kubadilishana wataalamu, uzoefu na mawazo.
“Lengo letu ni kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya operesheni kwani vituo vya mafunzo ya ulinzi wa amani vina nafasi muhimu katika dunia ya sasa, kwani vina jukumu la kuwajengea uwezo walinda amani ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kuleta utulivu na amani duniani,”amesema

Aidha amesema wamechagua nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na nchi hiyo kubarikiwa kwa mazingira mazuri na ina sifa zote zinazostahili kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu wa kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa 30 na kwamba fursa hiyo haijaja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya mchango mkubwa wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani duniani.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Brigedia Jenerali Itang’ar amesema mchango wa Tanzania katika agenda ya amani na usalama duniani unatambulika kimataifa, jambo ambalo limeifanya nchi kupewa heshima ya kuandaa mkutano huo muhimu unaotarajiwa kuwakutanisha wadau wa ulinzi wa amani kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema kuwa kupitia TPTC, Tanzania imekuwa ikichukua hatua za kuonyesha dhamira yake ya kuunga mkono juhudi za kimataifa za kuleta amani, na ndio msingi uliowezesha nchi kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria.
Kuhusu mchango wa Tanzania katika kusaidia mataifa ya Afrika yanayokumbwa na migogoro, amesema jukumu la usalama wa taifa hubaki kuwa la nchi husika, lakini kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Tanzania itaendelea kuwa tayari kutoa mchango wake pale itakapohitajika katika juhudi za kurejesha amani.


More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewaÂ
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77