May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mwenyeji mashindano ya binti Afrika

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

TANZANIA itashuhudia mashindano ya binti Afrika, kwa mara ya kwanza yenye lengo la kuiambia Tanzania na Afrika nzima kuwa, hapa ndipo itakapowekwa kambi ya mashindano hayo.

Mashindano ambayo yatasaidia kukuza lugha ya Kiswahili, kutangaza utu wa Mwafrika, lakini pia ni mashindano ambayo yana nia ya kuwafaya mabinti kutokujikondesha na kuwa na miili yao ya asili.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa KL International Agency, Alphonce Mkama amesema mashindano hayo kwa mara ya kwanza yatafanyika hapa nchini kwa lengo la kukuza lugha ya Kiswahili pamoja na kutangaza utu wa Mwafrika.
kondesha na kuwa na miili yao ya asili.

Mkurugenzi Mtendaji wa KL International Agency, Alphonce Mkama (katikati), akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa kutangaza eneo litakalofanyika shindano hilo.

“Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa zaidi na sisi kupitia Binti Afrika tunakwenda kutangaza lugha ya Kiswahili.

“Eneo hili la Kingazi, Tanzania ndio itakuwa kambi yetu kubwa na ndio ukumbi ambao utatumika kwa kila jambo ikiwemo kutembea kwa mikogo na maringo kwa mabinti hao

“Tunahitaji mabinti wenye maumbo makubwa na wenye nywele za asili na ngozi ya asili wasiojichubua, mashindano haya yatashirikisha Nchi zote za Afrika na wiki ijayo tutatangaza mawakala kwa Nchi zote.

“Mpaka Sasa Nchi 30 zimeshathibitisha kushiriki. Kambi itachukua miezi minne ili kutoa fursa kwa wageni kufundishwa lugha ya Kiswahili kupitia wakufunzi mbalimbali kutoa vyuo vyetu vikuu, Bakita na Bakiza kuja kukutana na washiriki wetu kuwafunza maneno mazuri ya kuvutia ya lugha ya Kiswahili,” amesema Mkama.

Mkurugenzi Mtendaji wa KL International Agency, Alphonce Mkama na Mkurugenzi wa Hoteli ya Kingazi, Nelson Mahenge wakionyesha mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi pamoja.

Nae Mkurugenzi wa Hoteli Kingazi, Nelson Mahenge amesema wamejiandaa kupokea ugeni mkubwa kutoka Nchi mbalimbali za Afrika na kuahidi kutoa huduma Bora zaidi

“Sisi tunapatikana maeneo ya Kijichi, Mgeni nani na nawakaribisha wageni, tupo tayari kuupokea ugeni huo, hapa tuna kila kitu ikiwemo malazi, chakula na vinywaji.

“Huduma zote zinapatikana, nawaombea kila la heri washiriki wote ambao watakwenda kushiriki katika mashindano hayo,” amesema Mahenge.