April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mjumbe bodi ya ushauri michezo Jumuiya ya Madola

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Tanzania imeteuliwa kuwa Mjumbe katika Bodi ya Ushauri Jumuiya ya Madola kwenye Michezo (CABOS).

Hatua hiyo inatokana na kuimarika kwa nyanja za diplomasia ikiwemo michezo katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Taarifa iliyotolewa na Waziri Chana na kulifikia dawati la Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizarani hapo imesema,

“Kwa uteuzi huo, Alli Mayay (Tembele) sasa anaiwakilisha Tanzania katika Bodi ya CABOS na kuwa Mjumbe mwakilishi wa Bara la Afrika huku ambapo kwa sasa Mayay ndiye Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Michezo nchini.”

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, CABOS ni chombo cha kumshauri Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na Serikali wanachama, kuhakikisha kunakuwepo ushirikishwaji thabiti wa Serikali na uwakilishi katika maendeleo ya sera na utekelezaji wake kwa kuzingatia maadili na matarajio yaliyowekwa ndani ya Mkataba wa Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Saidi Yakubu amesema uwakilishi huo, Tanzania imekidhi vigezo vya uanachama wa CABOS na itafanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na thabiti na wanachama wengine wapya na wanaorejea kutoka kila eneo la Jumuiya ya Madola kutoka Afrika, Asia, Karibiani, Amerika, Ulaya, pamoja na Pasifiki.

Tanzania inakuwa mjumbe CABOS kwa miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2023 hadi 2015

Michezo ya Jumuiya ya Madola inayohimiza michezo kwa maendeleo ya amani ulimwenguni, ilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Canada mwaka 1930.

Hadi sana inajumuisha mataifa kadhaa yaliyokuwa chini ya Utawala wa Uingereza hata hivyo nchi nne za mwisho kujiunga na Jumuiya ya Madola ni Rwanda, Msumbiji, Gabon, na Togo-hazina uhusiano wa kihistoria na Dola ya Uingereza.