Na. Mwandishi wetu,Gaborone – Botswana
Tanzania inajiandaa kufanya kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio Virus 2 (CVDPV2) katika Mikoa 6 inayopakana na nchi za Zambia na Burundi ambapo zoezi hilo limepangwa kufanyika mwezi Septemba na Novemba Mwaka huu 2023 ili kuwakinga watoto.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Agosti 31, 2023 katika Kikao cha Mawaziri kutoka nchi Tano za Afrika ambazo ni Zambia, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Tanzania.
Amesema, Nchi hizo zimepata mlipuko wa Ugonjwa wa Polio kwa wakati mmoja pamoja na nchi nyingine ambazo zipo katika tishio la kupata mlipuko wa ugonjwa wa huo.
“Kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Polio katika nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji, na kupatikana kwa mgonjwa mmoja wa Polio katika wilaya ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, Tanzania inajiandaa kufanya kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio Virus 2 (CVDPV2) katika Mikoa 6 inayopakana na nchi hizo kwa awamu mbili Septemba na Novemba”, amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema Tanzania ilishathibitishwa kwa kutokomeza ugonjwa wa Polio toka mwaka 2015 na hivyo iko makini katika kufuatilia tetesi na matukio yote yanayoashiria uwepo wa mlipuko wa ugonjwa huo nchini.
“Tuko makini kufuatilia tetesi za ugonjwa huu lakini pia utoaji wa kawaida wa chanjo ya Polio kwa watoto unaendelea ambapo hadi kufikia mwezi August, 2023 umefikia asilimia 94”, amesema Waziri Ummy
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania ilibidi kuendesha awamu Nne za kampeni ya chanjo ya Polio ya matone nchi nzima ili kumaliza tatizo hilo kwa watoto ambapo zaidi ya watoto milioni 17 walifikiwa.
Sambamba na hayo, Waziri Ummy ameelezea changamoto zinazopelekea kushindwa kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Polio ni pamoja na uwepo mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani za Malawi, Msumbiji, DRC, Burundi na Zambia.
“Hivyo katika kuhakikisha kuwa nchi inazuia milipuko ya ugonjwa wa Polio, Tanzania itaimarisha ufuatilia wa wagonjwa ikiwemo kuhakikisha Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii inapata ithibati kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuiwezesha kupima sampuli za ugonjwa wa Polio badala ya kupeleka nchini Uganda”, amesema Waziri Ummy
Amesema, Tanzania imepanga kutoa dozi ya Pili ya chanjo ya polio (IPV2) kwa mfumo wa utoaji wa chanjo wa kawaida.
Wakichangia katika mkutano huo wadau wa kutokomeza Polio Duniani wakiwemo UNICEF, GAVI, Gates Foundation na Rotary International wameshauri na kuziomba nchi za Afrika kushirikiana na wadau ili kutokomeza ugonjwa wa Polio duniani.
Mkutano huo umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 73 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Mjini Gaborone, Botswana.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito