Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi
TANZANIA inahitaji kukusanya chupa za damu 550,000 ili kuweza kujitosheleza katika benki yake ya damu,sanjari na kukabiliana na vifo, vikiwamo vya uzazi vinavyosababishwa na kutokwa na damu nyingi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya,Mendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na watoto nchini ya mwaka 2015/16 inaonyesha kati ya vizazi hai 100,000 kuna vifo 556 ambavyo ni sawa na asilimia 18 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15-49.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya ukusanyaji damu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) Dkt.Aveline Mgasa akitoa mada kuhusu kampeni ya ukusanyaji damu itakayoanza Septemba 21 hadi 25,mwaka huu hapa nchini.
Amesema kwa kipindi cha mwaka 2020 idara hiyo inatarajia kukusanya chupa 375,000 sawa na asilimia 70 ya mahitaji ya damu ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani(WHO) ili nchi iweze kujitosheleza damu inapaswa kukusanya asilimia moja ya wananchi wake.
Dkt.Mgasa amesema ili kufikia malengo ya ukusanyaji huo wa damu ambao umelenga kupunguza vifo vya wajawazito nchini, umewekewa utaratibu wa kila mkoa kukusanya chupa 150, halmashauri 185 nchini kila moja chupa 150, timu za damu salama kwa kila kanda chupa 500 na kwa kila hospitali ya kanda chupa 150.
“Kampeni hii kwa mwaka huu imepewa kauli mbiu ya ‘Damu Salama Uhai wa Mama’ kwani kushindwa kupatikana kwa damu salama kwa wakati tunapoteza robo tatu ya wajawazito kutokana na upotevu wa damu…hii ni sawa na kusema ikiwa vifo ni 18, vifo 6 ni kwa sababu ya ukosefu wa damu” amesema.
Amesema ni vyema jamii ikatambu umuhimu wa uwepo wa damu salama tukimaanisha damu iliyoandaliwa tayari kwa kutumiwa badala ya kuona tatizo na kuanza kutafuta ndugu wa kuchangia damu ambapo ili kuokoa maisha huenda akawekewa damu ambayo haijathibitishwa usalama wake.
Aidha Dkt.Mgasa amesema uhitaji wa damu kwa ajili ya kiama mama na watoto umeongezeka kama kundi lenye uhitaji mkubwa umeongezeka kutoka chupa 196,735 mwaka 2015 hadi chupa 309,376 mwaka 2020 sawa na asilimia 57.
Hata hivyo alivishukuru vyombo vya habari nchini kwa kuleta mapunduzi kwenye kampeni ya ukusanyaji damu mwezi Juni mwaka huu ambapo kampeni ililenga kukusanya chupa 24,800 na makusanyo yalikuwa chupa 18,075 sawa na asilimia 79.3 ya lengo.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo