May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Daudi Kaali akimkaribisha Waziri wa Kilimo Gerald Kusaya wakati wa kikao kazi baina ya Waziri Kusaya, Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa Mikoa kilichofanyika mjini Morogoro hivi karibuni.

Serikali yadhamiria kupanua wigo kilimo cha umwagiliaji

Na Aaron Mrikaria,TimesMajira Online, Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imedhamiria kupanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 694,715 za sasa hadi kufikia hekta 1,000,000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akifungua kikao kazi cha siku mbili baina yake, Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa yote nchini,mjini Morogoro, Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema Serikali imeamua kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo, uhakika wa chakula,kuinua kipato cha wakulima na kuongeza tija katika pato la taifa.

Kaimu Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Daudi Kaali akimkaribisha Waziri wa Kilimo Gerald Kusaya wakati wa kikao kazi baina ya Waziri Kusaya, Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa mikoa kilichofanyika mjini Morogoro hivi karibuni.


“Serikali imeweka malengo tuhakikishe kuwa ifikapo mwaka 2025 tunaongeza wigo wa miundombinu ya Umwagiliaji kufikia Hekta 1,000,000. maagizo haya ya serikali hakika tutayatekeleza kwa nguvu zote, bidii, na weledi mkubwa na tunahakika tutafanikiwa kwakuwa tuna raslimali watu,na fedha za kutosha kutekeleza miradi ya miundombinu ya umwagiliaji.”

Aidha Kusaya ameongeza kuwa nchi itakapokuwa na eneo kubwa la Umwagiliaji ndipo tutakapojihakikishia usalama wa chakula lakini pia tutajihakikishia upatikanaji wa tija katika suala la mazao ya chakula na yale ya biashara kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo hivyo, Tanzania haitakuwa na upungufu wa chakula na badala yake itauza nje mazao mengi ya biashara na mengine yatatumika kama malighafi katika viwanda vyetu hapa nchini.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Daudi Kaali amesema Tanzania ina eneo la Hekta milioni ishirini na tisa (29,000,000) zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na vyanzo vingi vya maji yakiwemo Mabwawa, Mito, Maziwa na Maji chini ya ardhi, kwahiyo kuna fursa kubwa ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Baadhi ya watendaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa mikoa wakimsikiliza katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (Hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika mjini Morogoro.

Tume ya Umwagiliaji imejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati katika mabonde yaliyoainishwa kama vile Bonde la Mto Rufiji na Bonde la Mto Ruhuhu na mengine mengi.

“Haya tumepanga kuyatekeleza,lakini utekelezaji wake unahitaji fedha kwahiyo mkakati wa serikali ni matumizi ya shilingi Bilioni 986.5 zinazotarajiwa kutumika katika ujenzi wa sekta ya umwagiliaji na kati ya hizo serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 80 na fedha nyingine zitatoka vyanzo mbalimbali ikiwemo ushiriki wa sekta binafsi,hataivyo Tume imepanga kuanzisha tozo mbalimbali katika miradi ya kilimo cha umwagilisaji ili kugharamia maendeleo ya sekta ya umwagiliaji.”

Kaali ameongeza kuwa kwa sasa nchi inahitaji malighafi nyingi za kilimo kutokana na ujenzi mkubwa wa viwanda hivyo ni vema sekta ya umwagiliaji ipewe msukumo ili ifikapo mwaka 2025 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iweze kutimiza malengo ya serikali kufikia hekta (1000,000.) za umwagiliaji.