May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TanTrade,UCSAF kutoa huduma ya Wi-Fi maonesho ya sabasaba

Na David John,Timesmajiraonline

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) pamoja na Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote( UCSAF) wamekutana na kufanya kikao cha jinsi ya kutoa huduma ya mawasiliano ya interneti WiFi (Wireless Internet) kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K Nyerere kwa kipindi chote cha Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (almaarufu Maonesho ya SabaSaba) yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni – 13 Julai, 2023.

Kikao hicho kimefanyika Juni 8.2023, katika Ofisi za TanTrade zilizopo jijini Dar es Salaaam kwa lengo la kuboresha na kurahisisha miundombinu ya mawasiliano ili kuwasaidia washiriki pamoja na watembeleaji kuweza kupata mawasiliano kwa njia rahisi na haraka zaidi katika kipindi chote cha Maonesho hayo.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara, TanTrade kwa Fortunatus Mhambe niaba ya Mkurugenzi Mkuu Latifa Khamis ameishukuru Taasisi ya UCSAF kwa kutoa huduma hiyo inayolenga kurahisisha mawasiliano na kuboresha Maonesho yawe na mvuto zaidi.

‘Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, natoa shukrani zangu za dhati kwa Taasisi ya UCSAF kwa kukubali kuboresha huduma za internet katika kipindi cha Maonesho, hivyo tunapenda kuuhabarisha Umma kwamba katika Maonesho hayo, huduma za Internet zitakuwa zimeimarishwa na kuboreshwa kwa ajili ya watembeleaji na waoneshaji na kuwarahisishia kuonesha biashara zao kwa njia rahisi zaidi’ alisema.

Kwaupande wake Mratibu kutoka UCSAF – Kanda ya Pwani Baraka Elieza amesema kuwa Taasisi ya UCSAF itahakikisha kuwa huduma za Internet zinakuwa nzuri na zenye kuleta tija katika Uwanja wa Maonesho na kuwafanya waoneshaji pamoja watembeleaji kuweza kufurahia huduma hizo kuanzia tarehe 28 Juni – 13 Julai, 2023.