Na Hafsa Omar, Kigoma
Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani ametoa siku tano kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kulipa fidia kwa wananchi wa Kidahwe waliopisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme(substation) cha Kidahwe kilichopo katika Kijiji cha Kidahwe, Kata ya Kidahwe Wilaya ya Kigoma vijijini, Mkoani Kigoma.
Agizo hilo amelitoa 27 Juni 2020, wakati akiwa kwenye uzinduzi wa kuanza malipo kwa wananchi ambao wameridhia kutoa ardhi yao kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Kupoza umeme cha Kidahwe.
Akizungumza kwenye tukio hilo amesema, zaidi ya shilingi milioni 700 zipo tayari kwaajili ya malipo ya wananchi 411 na kuwataka TANESCO kuanza mara moja kuwalipa wananchi hao na kuwapa siku tano tu kumaliza zoezi hilo.
“Niliacha maelekezo kwa waatalamu wetu kufanya kazi mbili, kazi ya kwanza ilikuwa kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi ambao wanapitiwa mradi wafanyiwe tathimini na kulipwa fidia zao na jambo hili tayari limeanza kufanyiwa kazi na jambo la pili ni kuanza matayarisho ya ujenzi wa mradi mkubwa huu,”amesema Dkt Kalemani.
Aidha, Dkt Kalemani amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kutoa maeneo yao kwaajili ya ujenzi wa kituo hicho kikubwa chenye uwezo wa kuzalisha umeme wa Kv 400, umeme huo ambao unatarajiwa kuondoa kero ya upatikanaji wa umeme Mkoani humo.
Dkt Kalemani amewataka wananchi watakaolipwa fidia hiyo kuzitumia vizuri fedha zao vizuri kwa kununua maeneo mengine na kujiendeleza kiuchumi.
“Mtakao lipwa fedha zenu msije mkazitumia vibaya hiyo hela halafu mkarudi tena TANESCO kudai hela nyengine hakuna hela nyingine hela ni hiyo hiyo utakayolipwa,” amesema.
Vilevile, amewataka TANESCO kuanzia tarehe 5 Julai waanze mara moja ujenzi wa kituo hicho, ili wananchi wa Kigoma waanze kupata umeme wa uhakika ambao utawasaidi kujenga uchumi wa Mkoa huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Emmanuel Maganga amewashukuru wananchi wote waliotoa maeneo yao kwaajili ya maendeleo ya Mkoa huo na amewahakikisha pesa zipo tayari kwaajili ya malipo yao.
Pia, amewatahadharisha wale wote watakaolipwa fidia hawataruhusia kuyatumia tena maeneo hayo kwani maeneo hayo yatakuwa ni mali ya Serikali kwasababu watakuwa tayari Serikali imeyalipia.
Katika ziara yake hiyo mkoani Kigoma, Dkt Kalemani pia ametembea kwenye kituo cha kupoza umeme cha Nguruka kilichopo katika kijiji cha Mganza na kuwataka TANESCO kumaliza ujenzi wa kituo hicho Julai mwaka huu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa