June 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yakamilisha Miradi kukamilisha upatikanaji wa Umeme Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Wananchi wa Wilaya za Gairo, Mpwapwa, Kongwa, Chamwino na Kiteto wanatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika zaidi kufuatia kukamilika kwa miradi ya kuimarisha mfumo wa usambazaji wa umeme iliyotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 10.5.

Miradi hiyo inahusisha Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station), Transfoma ya Kudhibiti Umeme (Automatic Voltage Regulator – AVR) yenye uwezo wa MVA 20 pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Zuzu hadi Mbande yenye urefu wa kilomita 92.

Akizindua miradi hiyo Juni 16, 2026 katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, Waziri wa Nishati,Deogratius Ndejembi, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi.

Amesema miradi hiyo imeleta maboresho makubwa katika mfumo wa usambazaji wa umeme katika ukanda huo, ambapo hapo awali hitilafu zilizokuwa zikitokea katika eneo moja zilisababisha wananchi wa maeneo mengine kukosa huduma ya umeme kwa muda.

“Kituo hiki kimeimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika. Hapo awali changamoto zilikuwa kubwa, hususan wakati wa mvua ambapo hitilafu katika wilaya moja ziliathiri huduma katika wilaya nyingine. Leo tunashuhudia matokeo ya uwekezaji huu kwa manufaa ya wananchi wetu,”amesema Ndejembi.

Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya nishati kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Taifa na mahitaji ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, alisema utekelezaji wa miradi ya umeme unaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi na kuchangia kufanikisha agenda ya maendeleo ya Serikali.

“Tunafarijika kuona kazi kubwa inayofanywa na TANESCO kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika. Hapo nyuma kulikuwa na changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo haya, lakini Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa kupitia TANESCO na matokeo yake yanaonekana wazi,” amesema Mgalu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, amewataka wananchi na wawekezaji kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo viwanda vya usindikaji, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi zitakazochochea maendeleo ya eneo hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange,amesema kwa muda mrefu wananchi wa Kongwa na maeneo jirani walitegemea njia moja ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Dodoma Mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kumeimarisha mfumo wa usambazaji wa umeme katika ukanda huo na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikiathiri upatikanaji wa huduma.

“Awali kulikuwa na njia moja ya kusambaza umeme inayopita katika wilaya tano tofauti. Kuongezeka kwa mahitaji ya umeme pamoja na fursa za uwekezaji kulianza kuleta changamoto katika utoaji wa huduma. Tangu miradi hii ilipoanza kufanya kazi, tumeshuhudia maboresho makubwa na changamoto zilizokuwa zikiathiri huduma zimepungua kwa zaidi ya asilimia 90,”amesema Twange.

Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuimarisha zaidi upatikanaji wa huduma ya umeme, kuongeza fursa za uwekezaji, kukuza shughuli za kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika Wilaya za Gairo, Mpwapwa, Kongwa, Chamwino na Kiteto.