May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yabeba ushindi wa jumla SHIMMUTA

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya SHIMMUTA baada ya kunyakua makombe tisa na kuibuka kidedea katika mashindano hayo ya mwaka huu yanayofanyika Mkoani Tanga.

Miongoni mwa makombe hayo TANESCO wamepata kupitia mchezo wa wavu wanaume na wanawake, kikapu wanaume na wanawake lakini pia imekuwa mshindi wa pili kwenye mchezo wa pete.

Hii ni mara ya nne mfululizo timu ya kikapu wanaume wanakuwa washindi na mara ya pili mfululizo kwa timu ya wavu wanaume inaibuka na ushindi.

Kwa upande wa michezo ya jadi TANESCO imeshinda mchezo wa bao wanawake, karata wanaume na mshindi wa pili bao kwa wanaume.

Mbali ya makombe hayo, TANESCO pia imepata medali saba ambapo Polycaps Ernest amekuwa mahindi wa tatu mbio za mita 100 na mita 200, Kulwa Mangala mshindi wa pili mita 1500, Grace Moshi mshindi wa pili mita 400 na 800, mshindi wa tatu mita 100, Imelda Hango 3000 wa tatu.

Akimwakilisha Meneja Mwandamizi Rasilimali Watu, Festo Mkolla ambaye pia ni Meneja Usimamizi na Utekelezaji Kazi TANESCO, ameishukuru Menejimenti kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Tito Mwinuka kwa kuona thamani ya michezo na kuipa kipaumbele.

Pia amewapongeza wanamichezo wa TANESCO kwa nidhamu, juhudi na hali ya kutetea Shirika kwenye mashindano ambayo wameionesha katika kuhakikisha kila mchezo wanaibuka na ushindi.

“Niwaagize viongozi wa timu ambazo hazikuibuka na ubingwa kuhakikisha mnaweka mikakati ili mwakani tuondoke na makombe yote” amesema Mkolla.

Kwa upande wa uongozi wa TANESCO umeahidi kuhakikisha yanafanyika mashindano ya Kanda za kitanesco ili kupata vipaji vipya vitakavyoongeza nguvu kwa wachezaji waliopo.