Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tanga yatakosa huduma ya umeme kuanzia Julai 9 hadi Julai 14, 2026, kupisha utekelezaji wa kazi muhimu za Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ya TANESCO, kukatika kwa umeme kutatokana na zoezi la uvutaji waya (stringing) katika njia ya umeme ya msongo wa kilovolti 33 eneo la Morogoro, ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
TANESCO imesema kazi hizo ni muhimu ili kuhakikisha mradi wa Chalinze–Dodoma unakamilika kwa wakati uliopangwa na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme nchini.
Huduma ya umeme itasitishwa kila siku katika kipindi cha kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni katika maeneo mbalimbali yatakayoathirika.
Maeneo yatakayokumbwa na ukosefu wa umeme ni pamoja na Mkulazi Feeder, likiwemo Kiwanda cha Mkulazi.
Pia, maeneo yanayohudumiwa na Turiani Feeder yataathirika, yakiwemo Wilaya ya Mvomero katika maeneo ya Wami Sokoine, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Mvomero, Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero pamoja na kata za Dakawa, Mvomero, Kinda, Maskati, Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mhonda, Kweuma, Diongoya, Mtibwa, Kanga, Mziha, Pemba, Kibati na eneo la Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR).
Katika Wilaya ya Kilosa, maeneo yatakayokosa umeme ni Dumila, Kitete, Ukaguru, Mfuru, Madudu, Mabana, Mateteni, Mbigiri pamoja na vijiji vya Tarafa ya Magole.
Kwa upande wa Mkoa wa Tanga, baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Kilindi ikiwemo Kikunde, Kwekivu, Ludewa, Tunguli, Namtoro na vijiji vya jirani vitaathirika, huku baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Gairo navyo vikikosa huduma ya umeme katika kipindi hicho.
TANESCO imewaomba wananchi na wateja wake kuwa na uvumilivu wakati wa utekelezaji wa kazi hizo na kuomba radhi kwa usumbufu utakaoweza kujitokeza.
Shirika hilo pia limetoa tahadhari kwa wananchi kutoshika wala kugusa waya wowote wa umeme uliokatika au ulioanguka chini, na badala yake kutoa taarifa kupitia namba ya huduma kwa wateja 180 ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

More Stories
Dkt. Kiruswa: Tanzania yageuka kitovu cha uwekezaji wa madini
TBA yakaribisha wawekezaji ujenzi makazi bora
Bodi ya Mkonge yahamasisha uwekezaji zao la Mkonge