May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA yatinga Zanzibar kuhamasisha upigaji kura hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetembelea visiwani Zanzibar kuendeleza kazi ya kuuelimisha Umma kuhusu shughuli zinazofanywa na shilika hilo.

Lakini pia, kuhamasisha kampeni ya ‘VOTE NOW’ ambayo inahusisha upigiaji wa kura kwa hifadhi ya Taifa Serengeti pamoja na Mlima Kilimanjaro,

Hifadhi hizo zinawania tuzo za ‘World Travel Awards’ katika kipengele cha Africa’s leading national park wakati Kilimanjaro ikiwania tuzo katika kipengele cha Africa’s leading tourist attraction.

Akizungumza na Redio Mjini FM Zanzibar leo, Afisa Uhifadhi Mkuu na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena amesema Rais Dkt. Samia Suluhu ndiye Guide namba moja hapa nchini, kutokana na kumuongoza Peter na kumzungusha katika maeneo mbalimbali kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ajili ya kutengeneza filamu ya Royal Tour.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na majukumu makubwa ya kuongoza nchi na kupata muda wa kufanya filamu ni kitu ambacho hatukukitegemea, tunasema ametushangaza.

“Lakini pia dunia ilikuwa katika janga kubwa la Uviko, watu walifungiwa lakini Dkt. Samia kuigiza katika hii filamu, hakuishia hapo lakini alitoka kwenda kuitangaza kwenye mataifa mbalimbali, ilifungua milango ya Utalii pamoja na uwekezaji,” amesema Catherine.

Amesema, Rais alipokwenda kuitangaza filamu ya Royal Tour nje ya nchi, alizungumzia vivutio vilivyomo nchini, pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana Tanzania.

Akizungumzia kuhusu Tuzo hizo Afisa Mhifadhi Mkuu, Happiness Kiemi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ameelezea namna ya kupigia kura Hifadhi za Taifa Serengeti na Kilimanjaro.

Happiness ameyasema hayo leo katika kipindi maalum kilichofanyika katika Redio Mjini FM Zanzibar, kwa ajili ya kuhamasisha na kuhakikisha Hifadhi hizo zinashinda tuzo za ‘World Travel Awards’.

Amesema, Hifadhi za Taifa zipo 21 lakini hifadhi hizo mbili zimechaguliwa kwenye kushindanishwa kidunia.

“Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inashindania Hifadhi Bora Barani Afrika, ambayo inashindana na nchi mbalimbali duniani. Hifadhi nyingine Kilimanjaro ambayo inashindania kivutio bora Afrika kwa Mlima Kilimanjaro,” amesema na kuongeza

“Kwa hiyo ni fursa kubwa ambayo tunaona kunakuwa na wageni wengi wanaofika Tanzania na wengine wengi wanatokea hapa Visiwani Zanzibar, kwa maana wanapata ‘Ndege ya moja kwa moja’ kutoka nchini mwao wanakuja Zanzibar, wanatembea kwenye fukwe lakini pia wanaenda maeneo ya Tanzania Bara,” amesema.

Hata hivyo amesema, ili kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia, Award hizo ni fursa moja wapo ya kuifanya Tanzania iendelee kujulikana zaidi duniani.

Amesema, Watanzania wakiweza kupigia kura hizo hifadhi mbili itawafanya wageni wengi wapate kujiamini mno kuwa Tanzania ni nchi sahihi kutembelea.

Amewataka watanzania wote, wadau wa utalii wapige kura kwa wingi ili hifadhi hizo ziwe kidedea na kuaminika kutokana na sifa za kipekee zilizojaliwa.

Ushindi huo utaongeza idadi ya watalii, mapato kwa taifa na kuongeza ajira kwa watanzania.