May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA yagundua eneo jipya lenye hazina ya nguzo za asili

Na. Mwandishi wetu

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika kuongeza mazao mapya ya utalii, limegundua eneo jipya lenye hazina kubwa ya Nguzo za Asili (Natural Pillars) zenye muonekano wa kuvutia ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Nguzo hizi zilizosimama mithili ya uyoga na kuvutia kwa macho zinasemekana zimetokana na kulika (kumomonyoka) kwa miamba yenye sifa tofauti kunakosababishwa na mwenendo mzima wa mtiririko wa maji na wakati mwingine pia zikichagizwa na upepo.

Ameyasema hayo Jana jijini Dar es Salaam Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha,Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godwell Meing’ataki, amesema muonekano wa nguzo hizo namna zilivyopangika unaweza kudhani kuwa kuna Mhandisi kazitengeneza na kuzinakshi,.

Amesema,kwa mara ya kwanza wanaona nguzo hizo walikuwa wakishuka na Helikopta katika eneo hilo hivyo walishangazwa na wingi wa nguzo hizi za asili (Natural Pillars) na kujua kuwa ndio hazina pekee iliyopo hapo.

“Tulipolizunguka eneo hili tuligundua lina utajiri mwingine wa masalia ya zana za mawe mithili ya zile zilizotumika nyakati za Zama za Mawe za Mwanzo,
Zana zinazoonekana katika eneo hilo jipya ni pamoja na mawe magumu yaliyotumiwa na binadamu wa mwanzo kusagia nafaka kwa ajili ya chakula au mizizi na magome ya miti kwa ajili ya tiba asilia, miamba iliyochongwa kiustadi mithili ya mikuki, mashoka na zana nyingine zilizotumika katika shughuli za uwindaji,”amesema na kuongeza

“Kwa mgeni mwenye kumbukumbu na ufahamu wa Nguzo za Asili (Natural Pillars) na zana za mawe zilizopo Tanzania anaweza kusema hapo ni Isimila, la hasha! ni moja ya eneo lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha takribani kilometa 70 kutoka Makao Makuu ya hifadhi hiyo yaliyopo Msembe,”amesema

Aidha, Amesema kwa utajiri wa nguzo, zana za mawe pamoja na sifa nyingine kedekede eneo hili linakidhi vigezo vya kuwa Geopark, kwani bara la Afrika lina Geopark mbili tu lakini tunashukuru ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha tuna eneo linaloweza kukidhi vigezo ambavyo vitatoa , fursa kwa hifadhi kutambulika zaidi kimataifa.

“Jitihada za kulitangaza eneo hili zimeanza ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ili kuvutia watalii wengi zaidi na wawekezaji, ukizingatia kuwa hiki ni kivutio kipya na muhimu kwa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha na hifadhi nyingine zilizoko Ukanda huu wa Kusini,”amesema.

Amesema TANAPA inatarajia kufanya taratibu za kuwaalika watafiti mbalimbali wa miamba, udongo na Malikale (Archiolojia) wa ndani na nje kubaini na kupata taarifa sahihi za malikale zilizopo, taarifa ambazo zitalitambulisha eneo hili kimataifa.

“Uimarishaji wa barabara unaenda sambamba na tathmini za kiutalii, kiikolojia na kiulinzi kubaini maeneo muhimu yatakayojengwa miundombinu ya kiutalii ili wageni wanapolitembelea eneo hilo wapate huduma ya malazi na chakula. Hatua hizi zikikamilika zitavutia watalii wengi na siku za kukaa hifadhini zinatarajia kuongezaka, siku zikiongezeka na mapato yanaongezeka kwa taifa”, amesema Meing’ataki