Na Penina Malundo,Timesmajira,Online
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ), kimetoa wito kwa jamii, asasi za kiraia kuona kuwa ni jukumu la kila mmoja katika jamii kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watoto.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 kila mwaka Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben amesema malezi ya watoto yanapaswa kuanza katika ngazi ya familia.
Amesema kupitia maadhimisho haya, serikali na wadau wanakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu uteuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.
“TAMWA inafanya maadhimisho haya siku ya kilele katika viwanja vya ofisi kwetu, kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tutekeleze ajenda 2040 kwa Afrika inayolinda haki za watoto,’ kauli mbiu hii inamlenga kila mtu katika jamii kuwajali watoto, kuwapenda na kuwalinda kwa namna yoyote ile,” amesema.
Amesema kulingana na kauli mbiu ya mwaka huu, ajenda ya mwaka 2040 ya Kamati ya Wataalamu ya Afrika kuhusu haki na ustawi wa mtoto wa Afrika ambapo Tanzania ni mwanachama.
Rose amesema kupitia maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa sera za taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma sahihi ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.
More Stories
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali