May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yamnasa anayedaiwa kumuweka kinyumba mwanafunzi

Na Jumbe Ismailly, TimesMajira Online, Ikungi

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida imefanikiwa kumkamata, mfanyabiashara wa kuuza sufuria, Ashirafali Ibrahimu Mohamed (51) mkazi wa Mtaa wa Upanga, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumweka kinyumba mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Dadu iliyopo Kata ya Dung’unyi, Wilayani Ikungi.

Mkuu wa TAKUKURU wilaya hapa, Erick Nyoni amesema, tukio hilo limetokea, Juni 14, mwaka huu ambapo mtuhumiwa alimshawishi mwanafunzi huyo wakati akiwa katika likizo ya lazima ya ugonjwa wa Covid-19 na kisha kwenda kuishi naye Dar es Salaam.

Nyoni amesema, mtuhumiwa huyo mwenye asili ya Asia ametiwa mbaroni baada ya kumkuta akiwa na mwanafunzi huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni Kijiji cha Puma, ambako ndiko walikofikia wakati akiwa njiani kwenda nyumbani kwa mwanafunzi huyo kutekeleza ahadi yake ya kumjengea nyumba ambayo alikwisha peleka jumla ya bati 32.

Baada ya mwanafunzi huyo kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, wazazi walitoa taarifa TAKUKURU na ndipo kwa siku hiyo kwa kushirikiana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi walijitahidi kumtafuta bila mafanikio.

“Tulipata taarifa zake toka tarehe 14/06/2020 kwamba alimshawishi binti huyo wakati wakiwa kwenye sherehe pale nyumbani kwao, akamdanganya kwamba waende naye kununua soda kwa ajili ya wageni lakini alipoondokana naye kwenye pikipiki yake aliendanaye mpaka Kijiji cha Puma kwenye nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Makuru na alimfungia ndani ya moja ya vyumba vya nyumba hiyo,” amefafanua Nyoni.

Inasemekana kuwa, Juni 15, mtuhumiwa aliondoka na mwanafunzi huyo na kwenda naye hadi jijini Dar es Salaam na kumfanya binti huyo kusitisha masomo yake na kwa kuwa mtuhumiwa ni mfanyabiashara, akawa anazunguka naye katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Lindi, Iringa, Mwanza, Shinyanga na Tabora.

Kutokana na mitego waliyoweka, walifanikiwa kupata taarifa za kiintelijinsia kwamba Septemba 21, mtuhumiwa Ashrafali atakwenda Ikungi kutekeleza ahadi ya kulipia gharama za kiwanja kitakachojengwa nyumba ya mwanafunzi huyo na ndipo walipofanikiwa kumtia mbaroni.

“Mtu huyu ni mhalibifu, kwani kabla ya kumshawishi mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha pili katika shule ya Sekondari Dadu, awali alimshawahi kumchukua binti mwingine na kumpeleka Dar es Salaam na baada ya kumtumia alimtelekeza na aliporudi alikwenda kumchukua tena binti mwingine ambaye pia alimtelekeza na ndipo aliporudi na kumchukua mwanafunzi huyo, ” amesema Nyoni.

Hata hivyo Nyoni amepiga marufuku vitendo hivyo kwani wasingependa kuvisikia tena na mtu yeyote atakayebainika kukatisha wanafunzi masomo na kuwapa mimba, hatua kali za kicheria zitachukuliwa dhidi yao.