October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yajitosa rushwa, kupitia manunuzi ya umma

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imezindua Mwongozo wa kuzuia rushwa kupitia manunuzi ya umma, huku huku ikisema taasisi za ununuzi zina kashafa kubwa ya kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa manunuzi .

Akizungumza leo jijini hapa kabla ya mwongozo huo kuzinduliwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema;

“Mwongozo huo una lengo la kudibiti mianya ya rushwa katika maeneo muhimu ya ununuzi na kuwahimiza wahusika kuzingatia taratibu ili kuhakikisha ubora na thamani ya ununuzi husika.

Pia unakusudiwa kutumika kama daraja kati ya wadau wa TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano,umoja na mshikamano katika kupambana na vitendo vya rushwa katika ununuzi wa umma.

“Mwongozo huu ni matokeo ya utashi na dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ambaye mara zote amekuwa mstari wa mbele katika kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini,” alisema Mbungo na kuongeza kuwa;

“Dhamira hii inadhihirishwa na uwepo wa mikakati mbalimbali ya kupambana na rushwa ukiwemo mikakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji awamu ya tatu wa mwaka 2017-2022 ambapo TAKUKURU ni miongoni mwa watekelezaji wa mkoa kati huu.”

Alisema mkakati huo unamtaka kila mdau katika eneo lake kuhakikisha amejiwekea mpango kazi wa kudhibiti vitendo vya rushwa katika eneo hilo,”alisema na kuongeza;

“Hivyo mwongozo huu unaainisha maeneo muhimu ambayo yanapaswa kupewa umakini wa kipekee wakati wa ununuzi ili kusaidia kubaini vitendo vya rushwa na kuvizuia mapema kabla ya kuleta madhara katika mchakato mzima wa ununuzi.”

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja muundo unaosimamia ununuzi wa ndani ya nchi na kimataifa, muundo wa ununuzi na usimamizi katika Taasisi Nunuzi na mchakato wa ununuzi wa bidhaa ,ujenzi na huduma za ushauri.

Maeneo mengine ni usimamizi wa mikataba na viashiria hatari vitokanavyo na utekelezaji wa ununuzi wa bidhaa, majenzi na huduma za ushauri,usimamizi wa ununuzi maalum na usimamizi wa uuzaji wa mali za Taasisi nunuzi.