November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Mbeya yatumia michezo na matamasha kufikisha ujumbe

Na Esther Macha ,Timesmajira Online, Mbeya

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya imekuja na mbinu ya kutumia michezo na matamasha kufikisha ujumbe wa kupinga vitendo vya Rushwa katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, mkuu wa Takukuru mkoa wa Mbeya Denis Manumbu amesema kupitia mbinu hizo wameweza kuwafikia watu zaidi ya 1500.

Amesema miongoni mwa wadau waliohusishwa ni vikundi vya skauti ambavyo waliwakilisha ujumbe wao kwa njia ya mabango pamoja na kutunga nyimbo za kupinga vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na athari zake katika ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

“Pia skauti hao walitunga ngonjera, waliandaa vipeperushi, ngonjera na mashairi ambavyo hivi vyote vinafikisha ujumbe kwa jamii, kwa hiyo kwetu sisi hayo tunaona ni mafanikio makubwa katika kutoa elimu kwa umma’’ amesema

Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema kuwa tamasha la michezo linalojumuisha michezo na maonesho mbalimbali litahitimishwa Janauri 22, mwaka huu katika uwanja wa Sokoine ambapo mgeni rasmi anatarajia kuwa naibu spika Dkt.Tulia Aksoni.

Aidha Kamanda huyo wa TAKUKURU amesema kuwa katika kuhitimisha tamasha hilo watamwalika mkuu wa mkoa, wabunge wote wa mkoa wa Mbeya pamoja na viongozi wa ngazi ya wilaya ili kushuhudia ujumbe utakaotolewa na washiriki siku hiyo.

‘’Tunategemea kuanza saa nne asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni ambapo tutaanza na maonesho ya kazi mbalimbali za skauti lakini pia tutakuwa na mashindano kwa ajili ya kuwatafuta washindi watatu na wanne na jioni tutawatafuta mabingwa ambao ni mshindi wa pili na wa kwanza’’ amesema

Kamanda TAKUKURU Mkoa wa mbeya Denis Manumbu akizungumza na waandishi wa habari