Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanznaia (TADB) na ‘African Gaurantee Fund’ (AGF) wametiliana randama ya makubaliano yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 20 kwa ajili ya kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wakulima wadogo, kati na wakubwa hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya utilianaji saini wa makubaliano hayo jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango. Dkt. Charles Mwamwaja mbali ya kupongeza makubaliano hayo, amesema yatakuwa chachu katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo.
“Kwa niaba ya Serikali , napongeza makubaliano haya kwani ni hatua kubwa kwa TADB kwa ushirika wao mkubwa na AGF, kwani utachochea maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo hususani kwa akina mama,” alisema Dkt. Mwamwaja.
Amesema kuwa makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuondoa changamoto ya dhamana katika mabenki hapa nchini na hivyo kuwezesha upatikanaji wa mikopo hiyo na kuwawezesha Watanzania wengi kushiriki katika sekya ya kilimo.
“Watanzania wamekuwa hawana dhamana ya kupata mikopo kwenye mabenki yetu, makubaliano haya yanaenda kuleta ahueni kwa Watanzania walio wengi, ambapo wamekuwa hawana dhamana na hivyo kuwafanya washiriki kikamilifu kwenye sekta hii inayoajiri watanzania zaidi ya asilimia 65,’’ alisema.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa AGF, Jules Ngankam amesema makubaliano hayo yamelenga kuongeza tija na kuifanya sekta ya kilimo itiliwe maanani zaidi ili kufikia maendeleo ya juu Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“TADB imekuwa benki muhimu sana kwa kuwa ni mahsusi kwa shughuli za kilimo tu, hivyo tunaamini makubaliano haya yatasaidia kuifanya sekta ya kilimo ipige hatua na kutoa mchango mkubwa zaidi ndani ya Afrika,’’ amesema Ngankam.
Ngankam amesema huo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa miradi ya AGF kwa Tanzania ambapo kufanikiwa kwake kutapelekea kufanyika kwa miradi mingi zaidi.
“Tunayo mikakati mingi ya kufanya kazi na Tanzania lakini tutatumia makubaliano haya kama sehemu ya kufanya miradi mingine kutegemeana na mafanikio ambayo yatapatikana,’’ amesema Ngankam na kuongeza kuwa mpango huo umelenga pia kuinua wanawake wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa mazao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine ameishukuru AGF kwa kufikia makubaliano hayo na pia ameihakikishia kuwa benki yake imejipanga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo sambamba na kuongeza uzalishaji na mnyororo wa thamani kwa mazao.
“Haya ni makubaliano ya kwanza kati ya TADB na AGF ambayo yamelenga kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wakulima wa wadogo, kati na wakubwa. Tunawahakikishia usimamizi mzuri na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya kilimo,” amesema Bw. Justine.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi