May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi ya TUWODO yafuturisha yatima Zingiziwa

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Tuinuke women Development Organization, (TUWODO)imefuturisha Futari kwa watoto wa Makundi maalum wa kituo cha AL Hidaya, kilichopo Zingiziwa wilayani Ilala.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Taasisi ya TUWODO Awena Omary, alisema dhumuni la kura Futari na watoto wa kituo hicho iiyotolewa na TUWODO ni kuonyesha upendo kwa makundi maalum nyakati hizi za mwezi wa Ramadhani waweze kufurahi kama jamii nyingine .

“Taasisi yetu ya TUWODO leo tumekula futari na watoto hawa wa kituo hichi ambapo kila mwaka TUWODO imeweka utaratibu wake kujumuika na watoto wa makundi maalum kisha kula futari pamoja “alisema Awena.

Mkurugenzi Awena Omary, aliwashukuru wadau mbalimbali waliomwezesha kufanikisha shughuli hiyo mpaka kufanikiwa jambo hilo kubwa kuwafanyia jamii.

Aliwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia jamii hasa watoto wa makundi maalum wa kituo hicho kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za malazi.

Alisema TUWODO inashughulikia maswala ya watoto na Kusaidia Jamii mbali mbali ikiwemo kuwawezesha na pia inasaidia Serikali katika sekta ya Elimu na Mazingira ikiwemo kupanda miti.

Alitumia fursa hiyo pia kuwapongeza Taasisi ya BUDEO,HCYWTF,DIWEO,TAHECO NA RECODO kwa ushirikiano wao wa pamoja katika kuunga mkono juhudi za TUWODO kufanikisha malengo yake.

Mlezi wa Kituo cha watoto wa Makundi Maalum AL Hidaya,Ziada Lafuteni aliwapongeza TUWODO kwa futari hiyo ambapo aliwaomba wadau wengine kuwasaidia Malazi kwa wanafunzi wa shule pamoja na kumalizia ujenzi wa majengo ya kituo hicho.

Kwa upande wake Waziri Shomari ambaye naye Mlezi wa kituo hicho alisema kituo hicho kina watoto 120 kati yao wanaume 55 na wanawake 65 ambapo kwa sasa kituo cha Al Hidaya kina changamoto ya sehemu ya kulala.