Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraonline,Dar
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO ) limepunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa fedha za uendeshaji kutoka serikalini, huku ikitekeleza kikamilifu falsafa ya Rais Dkt..Samia Suluhu Hassan ya 4R,ambapo wakati wa kuanza kwa mageuzi hayo, takribani asilimia 89 ya mahitaji ya shirika hilo yalitegemea fedha za Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse akizungumza Oktoba 16, 2026 jijini Dar-es- Salaam wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ameaema, shirika limetimiza mwaka wa nne mfululizo bila kutegemea fedha za matumizi ya kawaida ya Serikali (OC) kwa ajili ya uendeshaji wake, huku likifikisha miaka mitatu mfululizo likigharamia mishahara ya watumishi wake kupitia mapato ya ndani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hatua hiyo inaashiria kuimarika kwa uwezo wa STAMICO kugharamia shughuli zake za msingi, kupunguza shinikizo kwa bajeti ya Serikali na kuelekeza nguvu zaidi katika uwekezaji na upanuzi wa shughuli za kibiashara.
Shirika hilo limetoa gawio la jumla ya sh.bilioni 11 kwa Serikali, jambo ambalo, linaonesha mabadiliko katika uwezo wake wa kuzalisha faida na kurejesha sehemu ya matokeo ya uwekezaji kwa mwanahisa wake huku likiendelea kupata hati safi za ukaguzi wa hesabu, ishara ya kuzingatiwa kwa taratibu za uwajibikaji na usimamizi wa fedha.
Pia amesema, STAMICO imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya kiutendaji na kifedha, likiongeza mapato yake ya ndani kutoka sh.bilioni 1.3 katika mwaka wa fedha 2018/19 hadi sh.bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/26 sawa na ongezeko la asilimia 11,269 huku huku thamani ya mali za shirika ikipanda kutoka sh.bilioni 45 hadi sh.bilioni 360.
Hatua hiyo inaashiria mabadiliko makubwa katika uwezo wa shirika hilo kujiendesha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa ,huku likitekeleza kikamilifu Falsafa ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akiwasilisha mafanikio ya shirika hilo, Dkt. Mwasse anasema, ongezeko la mapato linaakisi mabadiliko yaliyofanywa katika usimamizi wa biashara, uwekezaji, uimarishaji wa miradi na matumizi ya rasilimali zilizopo ili kuongeza tija na ushindani wa shirika katika sekta ya madini hapa nchini.
Ukuaji huo unaonesha kupanuka kwa uwezo wa shirika katika kuzalisha mapato na kujenga msingi wa uwekezaji wa muda mrefu, hususan katika sekta ya madini ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania huku akisitiza umuhimu wa miradi ya kibiashara katika kuhakikisha shirika linaendelea kuwa na vyanzo endelevu vya mapato.
Amesema, STAMICO imepanua shughuli zake kwa kuingia katika mikataba mipya ya uchorongaji, ikiwemo mkataba wa muda mrefu na kampuni ya Geita Gold Mining (GGM), hatua inayolenga kuongeza fursa za kibiashara na kuimarisha mapato yatokanayo na huduma za kitaalamu katika sekta ya madini, huku idadi ya mitambo ya uchorongaji inayotumika katika shughuli za shirika imeongezeka kutoka mitambo mitatu hadi 18.
Vilevile, shirika limewekeza katika ununuzi wa mashine 15 za uchorongaji kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini, maarufu kama Artisanal and Small-scale Miners (ASM) ili kupata huduma zinazohusiana na shughuli zao za uchimbaji.
Uwekezaji huo unaonesha kuwa, shughuli za STAMICO hazilengi kuongeza mapato pekee, bali pia kupanua huduma zinazotolewa kwa wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wadogo ambao ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa madini nchini.Pia imeongeza pia idadi ya watumishi wake kutoka takribani 111 hadi karibu 800, kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji.

Hata hivyo Dkt. Mwasse amesema, mafanikio ya sasa yanapaswa kuunganishwa na uwekezaji wa kimkakati utakaoliwezesha shirika kuendelea kuwa na nafasi katika soko la madini kwa miaka ijayo,ambapo STAMICO imepata leseni 20 zinazohusiana na madini mbalimbali ya kimkakati yakiwemo bati, grafiti, lithiamu, madini adimu ya ardhini (rare earth elements), manganizi, kobalti, shaba, nikeli na dhahabu.Madini hayo yana umuhimu katika uchumi wa kisasa kutokana na matumizi yake katika viwanda, teknolojia, uzalishaji wa betri na nishati safi.
Sanjari na hayo Dkt. Mwasse amesema, shirika limeingia pia katika mikataba minne ya ubia inayohusisha madini ya kimkakati, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji na kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi yenye tija ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga vyanzo vya mapato vya muda mrefu, badala ya kutegemea mafanikio ya kifedha ya kipindi kifupi pekee.
Katika mkakati wake wa muda mrefu, STAMICO imeweka lengo la kuendeleza migodi mikubwa mitatu, ukiwemo migodi miwili ya dhahabu na mmoja wa madini ya msingi huku shirika linaendelea na hatua za maandalizi ya miradi hiyo ikiwemo kukamilisha tafiti zinazohitajika ili kuweka msingi wa utekelezaji wake.
“Iwapo miradi hiyo itatekelezwa kwa mafanikio, inaweza kufungua fursa mpya za ajira, kuongeza mapato ya shirika na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yatakayohusika.Utekelezaji wake utategemea kukamilika kwa tafiti, maandalizi ya uwekezaji na hatua nyingine muhimu za kitaalamu na kibiashara,”.


More Stories
Ndejembi aridhishwa na ujenzi wa Kituo cha Umeme Iganjo
Wizara ya Viwanda yabainisha utendaji wa taasisi zake
Tanzania yajipanga kuimarisha rasilimali watu kupitia TVET