

Na Joyce Kasiki,Dodoma
SERIKALI imeendelea kuchukua hatua za kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata elimu yenye ubora na fursa sawa za kujifunza kupitia Mkakati wa Nne wa Taifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031, unaolenga kuondoa changamoto zinazokwamisha ushiriki wao katika elimu.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Serikali imetoa vifaa saidizi vyenye thamani ya Sh milioni 730 kwa wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika shule za sekondari na vyuo vikuu nchini.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha elimu, kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kuwaandaa wananchi wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema katika kuboresha huduma za elimu maalum, jumla ya watumishi 2,058 wamepatiwa mafunzo, wakiwemo walimu wa elimu maalum 1,276, walimu wenye ulemavu 242 na walezi 346.
Aidha, Serikali imechapisha na kusambaza vitabu 22,600 vya Breli pamoja na vitabu 850,000 vyenye maandishi makubwa ili kurahisisha upatikanaji wa maarifa kwa wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu.
Katika hatua nyingine, Lugha ya Alama ya Tanzania imeingizwa kama somo la lazima kwa walimu tarajali, huku walimu tarajali 2,000 wakipatiwa ufadhili wa kusomea shahada ya elimu maalum ili kuongeza idadi ya walimu wenye uwezo wa kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema miongozo tisa iliyotolewa inaweka utaratibu wa kuboresha utekelezaji wa elimu jumuishi katika maeneo tofauti.
Ameeleza kuwa miongozo hiyo inahusisha mafunzo kazini, michezo, matumizi ya teknolojia saidizi, elimu ya awali, Lugha ya Alama ya Tanzania na lugha ya alama mguso, pamoja na hatua za kukabiliana na vikwazo vya kimazingira na mawasiliano vinavyoweza kuathiri ujifunzaji.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Juma Sekiboko, ametoa wito kwa wanafunzi na walimu kuhakikisha vifaa saidizi vinavyotolewa vinatumika ipasavyo ili viweze kuchangia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Mkakati huo unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa elimu jumuishi na kuweka mazingira yatakayowawezesha wanafunzi wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika elimu bila kukabiliwa na vikwazo vinavyoweza kuzuilika.

More Stories
STAMICO yaimarika, yatekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R
Ndejembi aridhishwa na ujenzi wa Kituo cha Umeme Iganjo
Wizara ya Viwanda yabainisha utendaji wa taasisi zake